PICHANI : Mh. Leonidas Gama akiwa na Waziri wa nchi OWM -TAMISEMI Mheshimiwa Kapteni Mstaafu George Mkuchika (Katikati)
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama, amewataka wataalamu wa Kilimo mkoani humo, kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake waende kwa wakulima kuwapa utalamu ili waweze kujikomboa katika lindi la umaskini kupitia sekta hiyo.
Bw. Gama aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu wa idara mbalimbali katika majumuisho ya ziara yake mkoani humo.
Alisema wataalamu wa kilimo na ufugaji hawana utamaduni wa kuwatembelea wakulima badala yake wanakaa ofisini hali ambayo inasababisha wakulima kujihusisha na kilimo cha mazoea.
“Hali ya kilimo katika Mkoa huu si mbaya sana lakini hali hii si kwamba inatokana na juhudi za wataalamu wetu wa kilimo hapana bali ni kutokana na wananchi wenyewe.
“Naomba kuanzia sasa, muende kwa wakulima ili waweze kulima kitaalamu na kupata mazao mengi hivyo kujikwamua kiuchumi,” alisema Bw. Gama.
Akizungumzia hali ya ufugaji mkoani humo, Bw. Gama alisema wananchi bado hawajanufaika na ufugaji kwani zipo changamoto nyingi ambazo zinaelezwa na wafugaji ikiwemo ukosefu wa chakula na ardhi ya malisho hali ambayo inasababishwa na wataalamu katika sekta hiyo kukaa ofisini.
Alisema wastani wa uzalishaji maziwa mkoani humo ni kati ya lita sita hadi nane ambao ni mdogo mdogo ukilinganisha nahali halisi ya mahitaji kwani wataalamu hao, wameshindwa kutoa mbinu mpya za ufugaji wa kitaalamu.
“Inaonesha kabisa wataalamu wetu wanakaa ofisini, hawaendi kwa wananchi kuwapa utaalamu, lazima wabadilike ili tuweze kuwakomboa wananchi na umaskini,” alisema
Alisema wataalamu hao wanapaswa kwenda kwa wananchi ili kutatua matatizo yao pamoja na kuwapa mbinu za kitaalamu juu ya kilimo na ufugaji ambazo zitawawezesha kufuga mifugo michache na kupata faida kubwa badala ya kufuga mifugo mingi wakati hakuna eneo la malisho.
No comments:
Post a Comment