KWA kutambua ukubwa wa sekta ya kilimo na mchango wake katika kuchangia pato la nchi na kutoa ajira serikali ya Tanzania imefanya juhudi kadhaa toka ilipopata uhuru mwaka 1961 wa kuipaisha sekta hiyo.Mikakati kadhaa yakiwemo matamko mbalimbali kwa ajili ya kukipa msukumo mkubwa kilimo iliasisiwa toka wakati huo, na mkakati wa hivi karibuni ni wa mwaka 2009, wa Kilimo Kwanza.
Mkakati huo hauna tofauti kubwa na mikakati iliyotangulia, lengo lake ni kuleta mapinduzi ya kijani ili kupunguza umaskini hasa wakulima wadogo ambao ni karibu asilimia 80 ya watanzania wapatao 44 millioni sasa.Aidha mkakati huu wa Kilimo Kwanza unalenga kukabiliana na ukosefu wa chakula wa mara kwa mara na kukuza uchumi kwa ujumla.
Tanzania ambayo hadi sasa haina viwanda vingi, kilimo kitaendelea kwa miaka mingi kuwa uti wa mgongo wa uchumi wake na mwajiri mkubwa. Mkakati unagusa uvuvi,ufugaji na urinaji.
Kilimo kinachangia pato la taifa kwa asilimia 26.7 huku asilimia 30 ya bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi zinatokana na kilimo. Asilimia 65 ya malighafi ya viwanda vyote vya ndani inatoka sekta hii ya kilimo.
Hata hivyo naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Christopher Chiza, anabainisha kuwa mkakati wa Kilimo Kwanza unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa nyenzo na upungufu wa elimu miongoni mwa watanzania.
Mkakati huu utafanikiwa kama kila mtanzania na sekta mtambuka zitatimiza wajibu wake kwa kiwango cha hali ya juu kabisa. Mikakati ya awali ilishindwa kufikia malengo kutokana na kukosa umakini.
Naibu waziri wa wizara ya kilimo na ushirika Christopher Chizya anaamini kuwa mkakati wa Kilimo Kwanza utafanikiwa na kwamba msisitizo utakuwa katika kuwapa elimu na nyenzo wakulima ili kuwawezesha kuendesha shughuli kwa ufanisi na tija.
Anasisitiza Chizya kuwa, mkakati utaweka pia msisitizo katika kuboresha miundombinu ya kilimo cha kisasa itakayosaidia wakulima na wenye viwanda kusafirisha mazao na bidhaa kwenda kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Tanzania ina kusudia ifikapo mwaka 2015 itakuwa na hekta milioni moja za kilimo cha umwagiliaji ambazo zitatoa asilimia 25 ya mazao yote ya kilimo.
Changamoto za kilimo kwanza
Taarifa ya waziri mkuu inabainisha kuwa mkakati unakabiliwa na changamoto kumi ambazo ni pamoja na migogoro ya ardhi, motisha kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwatafutia masoko, bei isiyokuwa ya uhakia ya mazao, miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
Changamoto nyingine ambazo ofisi ya waziri mkuu ilizitaja kuwa ni ukosefu wa maghala ya kuhifadhia mazao, ukosefu wa umeme maeneo mengi ya vijijini,barabara, reli na mawasiliano.
Mafanikio ya kilimo kwanza
Kutokana na kilimo kwanza kupewa kipaumbele takwimu zinaonyesha Tanzania inazalisha asilimia 95 ya mahitaji ya chakula chake.Aidha sekta hii inachangia asilimia 30 ya pato la nchi na pia kilimo kinachangia asilimia 65 ya bidhaa zote ambazo Tanzania inauza nje ya nchi na malighafi kwa viwanda vya ndani.
Jitihada zilizofanyika
Kutokana na umuhimu wa kilimo, serikali pia imeendelea kuongeza bajeti kwa wizara inayoratibu sekta hiyo kila mwaka ambapo 2004/2005 ilitengewa Sh157.7 bilioni, na mwaka 2005/2006 ikapandisha kufikia Sh233.3 bilioni na mwaka 2009/2010 ilifika Sh 722 bilioni.
Serikali pia imeendelea kutoa ruzuku kwa pembejeo ili kuwawezesha wakulima kununua kwa bei nafuu ili kusisimua kilimo. Kiwango cha ruzuku kimeendelea kupanda sawia na ongezeko la bajeti kila mwaka fedha. Hatua hiyo inalenga katika kuongeza tija na ubora wa mazao.
Aidha serikali iliongeza mtaji kwenye Benki ya Raslimali – TIB, kwa kuweka dawati maalum kwa ajili ya mikopo ya kilimo. Benki kadhaa pia zinatumika kutoa mikopo kwa ajili ya kilimo.
Nini kifanyike kuwezesha wakulima nchini?
Mkakati huu utafanikiwa tu kama serikali itawajumuisha wakulima wadogo ambao ndiwo wengi zaidi na wanalima eneo kubwa zaidi kuliko wakulima wakubwa. Kundi lipatiwa zana za kisasa yakiwemo matreka, mbole na zana nyingine za kilimo cha kisasa ili liondokane na jembe la mkono.
Tanzania inapaswa kuimarisha huduma za ugani na elimu ya kilimo cha kisasa hasa, kusaidia kujenga viwanda ya usindikaji ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuimarisha masoko.
Mbali na hayo kilimo cha umwagiliaji kitiliwe mkazo kama ilivyo kwa nchi kama Zimbabwe kwa kutoa mikopo ya riba ndogo.
Profesa Lucien Msambichaka, wa Idara ya Uchumi Chuo kikuu cha Dar es salaam anasema wakulima ni wanasayansi hivyo ili wabadilishwe mawazo yao lazima wajengewe mazingira sahihi.
Anasema kuwa wakulima wanatakiwa kuthaminiwa kwa kuwa na vyama vya ushirika imara katika kutetea haki zao na wawe na ujuzi wa kutosha kwa kupewa elimu na mafunzo bora ya kilimo pamoja na kuwapa zana bora za kilimo.
(Mwananchi,Wednesday, 21 September 2011 20:45)
No comments:
Post a Comment