Friday, August 5, 2011

Mradi wa Huduma za Fedha Vijijini – RFSP, wafanikiwa

RIPOTI iliyotolewa mwaka 2006 ilionyesha ni asilimia tano ya watu wa vijijini nchini Tanzania walikuwa wanauelewa na matumizi sahihi ya taasisi za fedha, asilimia 62 uelewa wa utunzaji fedha kwa kutumia mifumo isiyo rasmi na asilimia 33 hawakuwapo katika mfumo wowote wa utunzaji fedha.

Uelewa mdogo na matumizi duni ya huduma za fedha kwa nchi, siyo dalili njema kwa maendeleo ya uchumi wa kisasa. Katika kurekebisha dosari hiyo mwaka 2002 Tanzania ilianzisha Mradi wa Huduma za Fedha Vijijini – RFSP, chini ya ofisi ya Waziri Mkuu.RFSP ilianzishwa ili ya kusaidia taasisi ndogondogo za fedha vikiwemo vyama vya akiba na mikopo ( SACCOs) kuimarisha utoaji wa huduma za fedha vijijini.

Aidha mradi huu ambao ulikuwa unatekelezwa katika mikoa saba ulilenga pia katika kuwaongezea kipato watu maskini wa vijijini, mali, upatikanaji wa chakula na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kupitia SACCOS.

Hata hivyo RFSP, katika kutimiza malengo ambayo tumeyataja hapo juu ilitarajiwa pia kutoa mafunzo na elimu kwa watendaji wa SACCOs ya jinsi ya kuendesha vyama hivyo kwa kuzingatia utaalam na utawala bora.

Mradi huo wa miaka tisa katika tathimini yake iliyofanyika baada ya kukamilika Desemba 2010 ilibainika kuwa ulipunguza kiwango cha umasikini kwa asilimia 50.

Mafanikio haya siyo madogo na kwamba mradi huo kama utapanuliwa na kutandaa nchi nzima hapana shaka kasi ya kupambana na umasikini itafanikiwa katika muda mfupi ujao.

Taathimini iliyofanywa na taasisi ya Ecom Reseach Group inasifu mradi kuwa umefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini kwa wananchi waliokuwa katika eneo la mradi.

Mmoja wa maafisa wa taasisi hiyo walioshiriki katika tathimini ya RFSP,anasema kuwa mradi umefanikiwa kupungua kwa “ umaskini kwa wananchi katika vijiji husika kwa asilimia 50 kwa wanachama na asilimia 17.6 kwa wasio wanachama”.

Anasisitiza kuwa kiwango cha umasikini kwa wananchi kwenye maeneo ya mradi wasio wanachama bado ni cha kutisha ikilinganishwa na wanachama.Aidha anakiri kuwa RFSP imewajengea uwezo wananchi waliokuwa kwenye mradi, ambao wengi wao ni wakulima kwa kuboresha kilimo cha mazao, kuimarisha usalama wa chakula na watu kujiwekea akiba ya fedha.

Aidha RFSP imesaidia wananchi wengi kwenye maeneo ya mradi kuingia katika ujasiriamali kwa kuanzisha biashara mbalimbali kutokana na kupata mikopo kwa urahisi kutoka SACCOs na akiba zao binafsi.

Katika miaka tisa ya RFSP, pia wakulima wamesaidiwa kupata masoko ya mazao yao ya kilimo tena kwa bei ya soko. Chini ya mradi huu ndipo kumeanza mfumo wa soko wa stakabadhi ghalani, utaratibu ambao umekomesha dhuluma ya walanguzi wa mazao kwenye maeneo ya mradi.

Mfumo wa stakabadhi ghalani, pamoja na kumpatia mkulima bei ya haki ya mazao yake lakini inampatia fursa mkulima kutumia mazao yake, ambayo bado hayajauzwa kama dhamana ya kukopa katika SACCOs. Fursa ya kukopa, haikuwepo kabla yake. “ Mafunzo ya RFSP yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uongozi katika SACCOs 276 kwenye mikoa 7 na wilaya 23, ambapo wamefundishwa umuhimu wa viongozi na wanachama kuwajibikaji na utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa usahihi”, anasema afisa huyo.

Aidha katika kipindi hicho cha miaka tisa idadi ya SACCOS kwenye eneo la mradi iliongezeka kutoka 30 hadi 300 ilipofika Desemba 2010. Wanachama wa SACCOs, hali kadhalika waliongezeka kwa asilimia 70 na kwamba wananchi katika ujumla wao wameongeza uelewa vya kutosha ambapo uwekaji wa akiba umepanda kutoka asilimia 5 hadi 300.

Changamoto

Mtafiti kutoka Ecom Research Group, Deogratius Mushi anasema mradi huu ambao umegharimu dola za Marekani 27 millioni, mbali na mafanikio pia ulikuwa na changamoto lakini mmoja kubwa ni pale mfadhili mmoja alipojitoa katikati ya mradi na kusababisha naksi ya dola za kimarekani 2 millioni. Wafadhili wa RFSP walikuwa ni serikali ya Uswis na Shirika la misaada ya maendeleo ya kilimo (IFAD). OPEC baadaye ilijitoa.

Aidha kutokana na ufinyu wa bajeti, mradi huo ulifanya kazi katika eneo dogo la nchi licha ya kuwa umasikini umetandaa nchi nzima. Mradi ulikuwa katika baadhi ya wilaya za mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Dodoma, Singida na Kilimanjaro.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Pallangyo anahimiza kuwa maendeleo ya haraka ya sekta ndogo ndogo za fedha yatapatikana kwa kushirikisha sekta binafsi na kila mdau mwenye nia njema na kuongeza kuwa RFSP imeonesha njia.

Mafunzo kutoka RFSP

Mushi anasema matokeo ya RFSP yakisambazwa nchi nzima yanaweza kuleta mapinduzi katika sekta ya uchumi katika maeneo ya vijijini na taifa kwa jumla.

Anasema kwa kutumia mafanikio kwenye mikoa ya mradi wa RFSP tumeshuhudia umasikini ukipungua kwa asilimia 50 kwa wanachama wa miradi na asilimia 17 kwa wasiokuwa wanachama.
Hapana shaka kuwa RFSP imeonesha kuwa masikini wakipatiwa elimu wana uwezo wa kubadilisha uchumi na maisha yao kwa kasi kubwa.

Wakati umefika kwa benki na taasisi za fedha kuanza kutoa huduma katika maeneo ya vijijini kutokana na ukweli kuwa maeneo hayo ni hazina kubwa ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Chanzo;
Furaha Maugo,Mwanachi,(Wednesday, 03 August 2011)