Sunday, March 17, 2013

Wizara Kufufua Mifumo Asili ya Kilimo



Mfumo wa Kilimo cha asili aina ya Kiamba unaotumiwa na kabila la Wachaga.

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imeanzisha Mradi wa kufufua Mifumo muhimu ya asili ya kilimo Duniani (Global Importance Agricutural Heritage System- GIAHS) ili kuendeleza Kilimo cha asili (Oranic Farming) na kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la chakula Duniani (FAO) ambao unalenga kutambua mifumo ya asili na endelevu ya kilimo na ufugaji ili kumsaidia mkulima.
Afisa Mkuu wa Kilimo kutoka Idara ya Matumizi Bora ya Ardhi Bw.  Firmat Banzi
alisema mradi unagharimu zaidi ya dola laki mbili ambazo zimetolewa na Serikali ya Ujerumani.

Alisema kuwa katika Afrika Mashariki nchi ya Tanzania na Kenya ilichaguliwa kufufua mifumo hiyo kwa kuwa na sehemu muhimu za kilimo zanazotumia mifumo hiyo.
Aliongeza kuwa baada ya kuchanguliwa nchi ya Tanzani ilipendekeza mifumo mitatu ya kilimo asili ambayo ni Kihamba ambao hutumiwa na wachaga, Ndiva wa Wapare na Ngoro ambao hutumiwa na kabila la wamatengo.
Alifafanua kuwa mifumo hiyo mitatu ilifanyiwa utafiti na baadaye mfumo wa kichanga ulichaguliwa na kuanza kutumika. 
Aidha, alisema kijiji cha Chimbe juu kilichopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ndio kilichonufaika na mradi huo na sasa unafikia hatua ya mwisho katika utekelezaji wake.
Hatua hiyo imekuja baada ya tafiti mbalimbali kuonesha kushuka kwa bei ya zao la kahawa na kusema kuwa kilimo asili huongeza bei za mazao kwa kuwa mazao yanayolimwa hayatumii kemikali na badala yake hutumia mbolea ya asili kama vile samadi, aliongeza Bw. Banzi.
Mradi huo utasaidia kuboresha zao la kahawa kwa kutumia mbinu husishi za  kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.
Alifafanua kuwa  mradi unajumuisha utayarishaji wa vitalu vya miche, ukarabati wa mifumo asili ya umwagiliaji na utayarishaji wa mbolea za asili kama vile samadi.
Ili kuhakikisha mradi huu unaendelea Bw. Banzi alisema wameshirikisha wadau mbalimbali ambao watasaidia kuangalia kwa karibu maendeleo ya mradi, alitaja wadau hao kuwa ni Chama cha Ushirika KNCU cha Kilimanjaro pamoja na halmashauri ya wilaya.
Mifumo ya asili ya kilimo ilianza kupendekezwa dunia toka mwaka 2002 na baadhi ya nchi zimeanza kutumia mifumo hii, baadhi ya nchi hizo ni Japani, Philipino, China na Ujerumani.

Mifumo ya Asili ya Kilimo Kuendelezwa Kuinua Kilimo

Mazao yaliyostawi vizuri yakionyesha mojawapo ya aina ya kilimo Asili cha Mseto
Wadau wa kilimo, sera, mazingira, utawala, na mashirika ya kimataifa, wametoa wito wa kubaini mifumo asili ya Kilimo kwa kutambua mchango katika uhakika wa chakula na kipato.
Wito huo ulitolewa katika warsha iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyojumuisha wadau hao ili kutathmini mchango wa mifumo asili ya kilimo na changamoto zilizopo ili kuiboresha na kiendeleza.
Ilibainika kuwa Tanzania ina mifumo mingi ya asili ya kilimo na mifugo ambayo imedumu kwa taribani zaidi ya miaka 100 hadi 700.
Katika kipindi hicho, mifumo mingi imekumbana na mabadiliko ya hali ya hewa lakini imekabili na kudumu, hii inaonyesha kuwa kuna vitu vingi vya kujifunza katika mifumo hiyo.
Aidha, wadau wamependekeza mifumo ya asili ya kilimo na ufugaji kuingizwa katika sera kati ya zilizopo ili ipate nguvu ya kusimamiwa na kuendelezwa hasa ikizingatiwa umuhimu wake katika kuimarisha usalama wa chakula na kipato kwa kaya na taifa kwa ujumla.

Pia wametaka mashirika ya kimataifa yaendelee kuchangia kwa rasilimali uendelezaji wa mifumo asili endelevu kwani manufaa yake ya mazingira ni ya ulimwengu.

Afisa Mkuu wa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Firmat Banzi alisema kuwa mifumo asili ya kilimo ina haja ya kuendelezwa ili kuboresha na kuimarisha maarifa asili kuwezesha ushiriki wa wakulima katika utunzaji wa mifumo hiyo.
Alifafanua kuwa uendelezaji wa mifumo hiyo utawapa fursa wakulima kuweza kushiriki kikamilifu katika kilimo wakiwa na uhakika wa kupata mazao mengi kuweza kujitosheleza kwa chakula na kujiongezea kipato pamoja na kuboresha hifadhi ya mazingira hasa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Washiriki kwa pamoja wamepitisha azimio linalotambua mchango wa mifumo ya asili ya kilimo na ufugaji na wametoa wito wa kubaini mifumo asili iliyopo nchini, kutathmini mchango wake na changamoto kwa lengo la kuiboresha na kuiendeleza.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI ZA VYAKULA MIKOANI



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAWIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA


TAARIFA KWA UMMA  KUHUSU BEI ZA VYAKULA MIKOANI


UTANGULIZI: 

Tulianza msimu huu 2012/13 tukiwa na ziada kidogo ya chakula na kwa kujitosheleza kwa asilimia 113. Msimu huu, tofauti na msimu uliopita hatukuzuia wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi.

Pamoja na uzalishaji tuliokuwa nao katika maeneo kadhaa ya nchi kulikuwepo na maeneo ambayo uzalishaji wake haukuwa wa kuridhisha kutokana na hali mbaya ya hewa na hivyo kuwa na upungufu wa chakula.  Upungufu huu unajidhihirisha kutokana na kupungua  kwa uingiaji na upatikanaji wa vyakula sokoni, hususani unga wa mahindi ambacho ni chakula kikuu        na  bei ya soko kupanda  sana kwa viwango vilivyo juu ya bei ya wastani nchini.

Uchambuzi wa bei za vyakula unaonesha kwamba bei ya wastani ya mahindi kitaifa ni shilingi 675 kwa kilo.  Aidha, bei ya mahindi katika masoko ya miji mkuu ya baadhi ya mikoa iko juu ya wastani.  Kwa mfano, bei ya Dar es Salaam tarehe 28 Novemba, 2012 ilifikia shilingi 750 kwa kilo, Mwanza shilingi 825, Moshi shilingi 700, Tanga shilingi 785, Tabora shilingi 750 na Mtwara shilingi 735.  Aidha, unga wa sembe uliuzwa kati ya shilingi 1,100 na shilingi 1,500 kwa kilo, mwezi Desemba 2012.

Hali ilivyo katika maeneo mengi ya nchi ni kwamba, viwango vya upatikanaji wa chakula vinatofautiana katika maeneo mbali mbali.  Wakati mikoa minane (8) ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro ilikuwa na ziada ya chakula, mikoa saba (7) ya Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida na Dodoma ilikuwa na hali ya utoshelevu tu na mikoa sita (6) ya Shinyanga, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dar es Salaam ilikuwa na uhaba wa chakula.

Kutokana na upungufu wa chakula kuzidi kujitokeza, mwezi Oktoba, 2012, Serikali, kupitia Kamati ya Maafa iliidhinisha mgao wa tani 18,417.8 wa chakula cha njaa kutoka katika maghala ya Hifadhi ya Chakula ya Taifa (National Food Reserve Agency) kwenda katika Halmashauri 35 za mikoa 12 zilizobainika kuwa na upungufu mkubwa wa chakula.  Mikoa iliyopewa chakula cha njaa ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

Kutokana na hali ya upungufu wa chakula kuzidi kuendelea na kujitokeza kwa majanga mengine kama mafuriko, Serikali iliidhinisha mgao wa nyongeza ya chakula hadi kufikia tani 26,958.300 kwa Halmashauri zilizokuwa  na mahitaji makubwa ya chakula cha msaada.  Aidha, upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo yanayozalisha nafaka kwa wingi umesababisha kupungua kwa chakula kinachosambazwa katika soko hivyo kufanya usambazaji wa chakula kutolingana na mahitaji ya soko. Hali hii imesababisha kupanda kwa bei ya mahindi na unga wa  mahindi katika baadhi ya masoko hususan  ya mijini. Ili kukabiliana na hali hiyo Serikali imechukua  hatua zifuatazo:-
(i)      Kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yaliyokuwa na upungufu wa chakula.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye upungufu wa chakula Serikali iliendelea kuongeza mgao wa chakula cha msaada kutoka tani 18,417.8 hadi kufikia  tani 28,250.300. Hadi kufikia mwezi Januari, 2013 jumla ya tani 19,040.865 za mahindi zilishachukuliwa. Aidha, jumla ya tani 9,209.435 bado hazijachukuliwa na mikoa iliiyopewa mgao wa nyongeza. Mikoa ambayo bado haijachukua nyongeza hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Mbeya na Mara. Kiambatisho Na. 1
(ii)    Kuuza tani 40,000 za mahindi kutoka kwenye ghala la Taifa kwa ajili ya kushusha bei ya unga wa mahindi.

Serikali imeidhinisha kuuzwa tani 40,000 za mahindi kutoka katika ghala la chakula la taifa ambapo tani 20,000 zitauzwa kati ya mwezi Januari na Februari, 2013. Kwa bei ya shilingi 450 tu kwa kilo. Kiasi kingine cha tani 20,000 kilichobaki kitauzwa kuanzia mwezi Machi katika maeneo yatakayobainika kuwa na upungufu wa chakula na bei kuendelea kupanda. Mgao Kimkoa ni kama inavyoonyesha kwenye Kiambatisho Na. 2.

2.        UTARATIBU WA KUUZA MAHINDI KWA WASAGISHAJI
Mikoa yenye bei ya mahindi iliyo juu ya bei ya wastani kitaifa ndiyo iliyopewa mgao. Mikoa hiyo na mgao wake katika mabano ni kama ifuatavyo:  Arusha (tani 1100), Dodoma (tani 400), Kilimanjaro (tani 400), Lindi (tani 400), Mara (tani 900) , Manyara (tani 800), Morogoro (tani 400), Mwanza (tani 2500), Shinyanga (tani 1029), Singida (tani 500), Tabora (tani 1000), Tanga (tani 700), Mtwara (tani 600) , Pwani (tani 700), Simiyu (tani 1971) na Dar es Salaam (tani 6400).
Utaratibu unaotumika kuuza mahindi kwa wasagishaji ni kama ifuatavyo:
  i.        Mikoa imeelekezwa kuteua wasagishaji waaminifu wenye nia na uwezo wa kusagisha unga kwa ajili ya kuuza kwa walaji kwa bei elekezi iliyopangwa na mkoa ambayo ni kati ya shilingi 750 hadi 900 kwa kuzingatia gharama za usafirishaji.
 ii.        Wasagishaji walioteuliwa wanatakiwa kukidhi vigezo vilivyowekwa kama vile, uwezo wa kulipa fedha za mahindi ndani ya muda uliopangwa, uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mahindi anachonunua, uwezo wa kusagisha, kufungasha na kusambaza unga ndani ya siku saba kuanzia siku aliyochukua mahindi, pamoja na kukubali kuuza kwa bei elekezi.
iii.        Wasagishaji walioteuliwa na mikoa watapewa vibali na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ili waweze kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala kama watakavyopangiwa.
iv.        Mikoa itaingia mikataba na wasagishaji walioteuliwa na kusimamia utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta manufaa yaliyokusudiwa.


v.        Mikoa itachukua hatua kwa msagishaji ambaye atabainika kutumia vibaya kibali alichopewa, kama vile kuuza kibali hicho kwa msagishaji mwingine, kusafirisha na kuuza mahindi au unga kwenye maeneo tofauti na aliyopangiwa, kutosagisha na kuuza unga ndani ya siku saba kwa mujibu wa mkataba.
3.   UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUPUNGUZA BEI YA UNGA KWA WALAJI
Mikoa iliyopewa mgao imeelekezwa utaratibu wa kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hadi kufikia tarehe 14 Januari, 2013 jumla ya mikoa 11 kati ya Mikoa 16 ilikuwa imewaslisha orodha ya wasagishaji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Mikoa hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani,Tanga na Dar es Salaam. Mikoa ambayo haijawasilisha orodha ya wasagishaji ni Mwanza, Tabora, Shinyanga, Mara. 

Kuendelea kuchelewa kuwasilisha orodha ya wasagishaji kunasababisha kuchelewesha zoezi zima la utoaji wa mahindi, usafirishaji, usagishaji na hivyo kuchelewesha unga kuingia sokoni hali inayosababisha bei kuendelea kupanda.  Mikoa hiyo inaagizwa kuwasilisha orodha ya wasagishaji ndani ya siku saba kuanzia sasa.  Jumla ya wasagishaji 127 tayari wameshapewa vibali vya kununua mahindi yanayofikia tani 12,520.00 ambapo tani 7,858.291 zimeshalipiwa na uchukuaji unaendelea lakini kasi ya kulipia na kuchukua ni ndogo. Orodha ya Wasagishaji kama ilivyowasilishwa na mikoa na kiasi walichoidhinishiwa kununua imeoneshwa katika Kiambatisho Na.3.

Serikali inawaagiza Wasagishaji wote waliopewa vibali vya kununulia mahindi kuhakikisha wanalipia na kuchukua kiasi chote cha mahindi kama walivyoidhinishiwa katika vibali vyao ndani ya siku saba kuanzia sasa, vinginevyo Serikali italazimika kufuta vibali hivyo na kuvigawa upya kwa Wasagishaji wengine katika mikoa husika wenye nia thabiti ya kufikisha unga sokoni.
4.  USIMAMIZI NA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI
Wakuu wa Mikoa  na Wilaya wanaagizwa kusimamia na kufuatilia kikamilifu utekelezaji wa zoezi hili kama ilivyoelekezwa. Aidha, mikoa inatakiwa kuweka mfumo mzuri wa usimamizi na usambazaji wa unga unaotokana na mahindi yaliyonunuliwa kutoka katika ghala la Serikali ikiwa ni pamoja na kuwafahamisha wananchi maeneo ambayo unga huo unapatikana pamoja na bei elekezi iliyopangwa na mikoa.
Katika ngazi ya Taifa Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa mkakati huu katika mikoa yote iliyopata mgao wa chakula cha njaa au mgao ulitolewa kwa wasagishaji kwa ajili ya kupunguza bei ya unga katika masoko ya mijini.
5. MWISHO
Kwa kuwa maghala ya Dar es Salaam (Kipawa), Arusha, Dodoma na Shinyanga yana upungufu wa akiba ya chakula kulinganisha na mahitaji ya sasa katika maeneo hayo,  Serikali inaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yenye akiba ya kutosha kwenda katika maghala yenye upungufu ili kurahisisha usambazaji wa chakula katika maeneo yenye upungufu. Tunaendesha zoezi hili la kuhamisha  chakula kwa kutumia Shirika la Reli (TRL) , Jeshi la Wananchi na wasafirishaji binafsi ili kuhakikisha kwamba chakula kinafika haraka.