Thursday, May 9, 2013

UFUGAJI WA NGURUWE

Photo: Pig peering over a wall
“Ufugaji wa Nguruwe ni lazima uwe wa kisasa ili kupata mazao bora. Unaweza kupata kila unachohitaji wewe, familia na hata ndugu zako kutokana na ufugaji wa nguruwe”, anasema Bwana Lomaiyani Molel kutoka Arusha. Jamii nyingi hapa Tanzania huchukulia nguruwe kama mnyama mchafu na asiyefaa kuwa karibu naye na hata kwa matumizi kama lishe. Zaidi, nyama yake inapendwa na haina madhara kwa afya na inapendekezwa kuliwa zaidi kuliko nyama nyekundu. Unaweza kuanzisha mradi wa nguruwe kwa gharama ndogo lakini baada ya kipindi cha miezi tisa tu ukaanza kujipatia kipato kutokana na ufugaji huo.


Ufugaji
Kwa kawaida nguruwe wanafugwa na watu wa kada zote, wafugaji wadogo wadogo na hata wakubwa. Aina hii ya ufugaji huweza kumpatia mkulima kipato pamoja na lishe kwa familia, na hauhitaji gharama kubwa.

Banda

Nguruwe wanahitaji kuwa na banda lililojengwa kwa vifaa nafuu. Unaweza kutumia mchanga na simenti kuweka sakafu, ama ukatumia udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kuweka sakafu. Ukubwa wa banda unategemeana na idadi ya nguruwe unaotaka kufuga. Mita 3 kwa mita 2.5 zitawaweka guruwe 8-10 wanaonenepeshwa kwa soko au nguruwe jike mmoja na nguruwe dume mmoja.

Malisho

Ulishaji wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula kulingana na mazingira wanayofugwa. Unaweza kuwalisha kwa kutumia majani laini ya aina mbalimbali, na pia hulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka (pumba). Unaweza kuwalisha kwa kutumia mashudu au pumba aina ya Wheat Poland. Pia unaweza kuwalisha kwa kutumia mabaki ya jikoni.

Kuzaliana


Nguruwe hubeba mimba kwa kipindi cha siku 114, ambazo hugawanyika kwa miezi 3, wiki 3 na siku 3. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kuzaa watoto 6 hadi 14 kwa mara moja. Watoto wa nguruwe (piglets) huanza kula chakula cha kawaida wanapofika umri wa mwezi mmoja na nusu mpaka miezi miwili. Endapo nguruwe watapata matunzo mazuri, baada ya miezi 8 wanakuwa na uzito kati ya kilo 50-70 na wanaweza kuuzwa.
 
Matunzo

Baada ya nguruwe kuzaa anatakiwa kupatiwa chakula cha kutosha na cha kutia nguvu ili kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wake. Watoto wa nguruwe wachomwe sindano ya madini ya chuma (Iron injection) baada ya siku moja au mbili toka kuzaliwa. Hii ni muhimu sana vinginevyo wanaweza kufa wote. Kata meno (tooth clipping) baada ya miezi mitatu. Unaweza kuhasi madume (castration) baada ya miezi miwili.


Magonjwa yanayoathiri nguruwe

Kuna aina nyingi za magonjwa yanayoshambulia nguruwe, lakini yapo yale yaliyozoeleka ambapo ni lazima kukabiliana nayo ili kuwa na ufugaji wenye tija.


Ugonjwa wa miguu na midomo

Ugonjwa huu huathiri nguruwe sehemu za miguu na midomo. Ni ugonjwa ambao hushambulia nguruwe mara kwa mara hasa wasipokuwa na matunzo mazuri. Ugonjwa wa miguu na midomo, hudhoofisha nguruwe kwa haraka sana, ikiwa ni pamoja na kupungua uzito.



Chanjo:
Chanjo kwa ajili ya ugonjwa wa midomo na miguu (FMD vaccine) hutolewa kila baada ya mwaka mmoja. Hii inasaidia kuwaweka nguruwe wako katika hali nzuri zaidi bila kushambuliwa na magonjwa hayo.


Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba halisi. Inapotokea nguruwe wakawa wameshambuliwa kinachofanyika ni kutibu magonjwa nyemelezi kwa kutumia antibiotics.
Homa ya Nguruwe (Swine fever)

Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe huenea kwa haraka sana miongoni mwa makundi ya nguruwe, na huua kwa haraka sana, lakini hauna madhara kwa binadamu na hauambukizwi kwa binadamu. Nguruwe walioambukizwa waanshikwa na vindonda ama mapunye kwenye ngozi. Pia masikio na ngozi huwa mekundu.

Chanjo: Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba. Kinachofanyika mlipuko unapotokea ili kuwa salama ni kuwateketeza nguruwe wote walioathirika na kuanza upya. Unaweza kuteketeza kwa kuwachoma moto.

Muhimu: Baada ya kuwateketeza nguruwe wagonjwa, safisha banda kisha nyunyiza dawa aiana ya Acon au Ectomin, na uache banda wazi kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kuweka nguruwe wengine.
Ugonjwa wa mapafu (Pneumonia)


Huu ni ugonjwa unaoshambulia sehemu za koo na mapafu ya nguruwe, ambapo husababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria (Secondary bacterial), joto kupita kiasi, vumbi na gesi inayotokana na madawa makali.



Tiba:
Homa ya mapafu kwa nguruwe inatibika kwa kutumia antibiotics. Pamoja na kuwaweka wanyama sehemu safi, isiyo na baridi kali au joto la kupitiliza kiwango.

Kimeta (Anthrax)


Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Bacillus anthracis, wadudu hawa wanabaki kuwa hai kwa muda mrefu na wanaweza kuwa kwenye udongo wakiwa hai kwa kipindi cha miaka mingi.


Chanjo:
Chanja nguruwe wako dhidi ya kimeta kama utakavyoelekezwa na wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.

Tiba:
Unaweza kutibu nguruwe wako kwa kutumia dawa aina ya Penisilin au Oxytetracycline.

Muhimu:
Homa ya nguruwe ni lazima iwekewe karatini kwa sababu husambaa kwa haraka sana. Nchini Tanzania mlipuko wa homa ya nguruwe umekuwa ukitokea mara kwa mara maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na katika mkoa wa Mbeya.

1 comment:

  1. naomba kujua, mnyama anapopata homa ya Nguruwe akiliwa na na binadamu au mfugo ka mbwa una madhara gani kiafya.
    badala ya kuwatekeza kwanini wasiwe chakula cha viumbe wengine kama kwa binadamu nayo ni tatizo?

    ReplyDelete