Friday, September 24, 2010

WAJIBU WA VIJANA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

UTANGULIZI
Mapambano dhidi ya rushwa si ya Serikali au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) peke yake bali ni ya jamii nzima. TAKUKURU ina jukumu la kuongoza na kushirikisha jamii nzima katika mapambano haya wakiwemo vijana. Kutokana na ukweli kwamba vijana ni rasilimali ya taifa, watendaji wa siku zijazo na chuchu ya mabadiliko katika jamii, wanao umuhimu wa kipekee kuleta mabadiliko ya kijamii hasa katika kubadili mtazamo wa jamii kuhusu rushwa kutoka kwenye matazamo kuwa rushwa ni sehemu ya utamaduni na jambo linalokubalika na kuiona rushwa kuwa ni kosa lisilotakiwa kuvumiliwa kwa namna yoyote kutokana na athari zake kwa jamii.

MAANA YA RUSHWA
Rushwa ni neno pana ambalo haliwezi kutosheleza na tafsiri moja japokuwa limekuwapo tangu zamani sana. Watu wengi wamejaribu kutafsiri rushwa katika mitazamo tofauti. Tunaweza kutafsiri rushwa kuwa ni:-
Kitu chochote cha thamani kinachotolewa au kupokelewa kinyume na sheria ili kupata au kutoa huduma.
Matumizi mabaya ya madaraka ya mtumishi wa umma ili kupipatia maslahi binafsi.

Rushwa hujumuisha kupindisha sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa manufaa ya mtu binafsi na ya wale wanaopenda kutumia fedha au kitu chochote ili mtoe huduma afanye wanavyotaka wao.

SABABU ZA KUWEPO KWA RUSHWA
Kuna sababu mbalimbali zinazosababisha au zinazochangia kuwepo kwa rushwa ambazo ni:-
Mmomonyoko wa maadili miongoni mwa viongozi, watumishi wa umma na jamii kwa ujumla.
Elimu ndogo kwa wananchi juu ya haki na wajibu wao wa kupata huduma mbalimbali.
Ubinafsi na tabia ya uroho wa mali ili kujinufaisha na kujilimbikiza mali au utajiri.
Urasimu katika kutoa huduma mbalimbali.
Watu kutumia njia ya mkato kukamilisha na kutatua matatizo yao au kupata huduma.
Mishahara midogo kwa wafanyakazi wa serikali na taasisi zingine.
Watu wasio waadilifu kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nyadhifa za juu na hivyo kusababisha kukosekana kwa utashi wa kisasa.
Ubutu wa sheria mbalimbali.
Ukosefu wa vitendea kazi.

ATHARI ZA RUSHWA
Rushwa husababisha madahara mengi katika jamii ambayo huathiri nyanja zote kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiasa.
Baadhi ya athari hizo ni:-
Kushuka kwa pato la Taifa.
Kuongezeka gharama zisizo za lazima katika miradi mbalimbali zinazosababisha wananchi kukosa huduma muhimu za kijamii.
Kuvusha nyara za serikali, madini na biashara ya madawa ya kulevya.
Huathiri utekelezaji wa majukumu ya serikali yao mfano kuacha kutoa ushirikiano kwa serikali.
Husababisha wananchi kukosa imani na serikali yao mfano kuacha kutoa ushirikiano kwa serikali.
Hukwamisha utoaji wa haki.
Huogofya wawekezaji.
Huhamisha rasilimali za nchi kwenda kwa wananchi wachache walio na uwezo.
Husababisha kuongezeka kwa maovu katika jamii.
Husababisha kuongezeka kwa maambukizi ya UKIMWI.
Husababisha kuwa na viongozi wasiofaa.
Husababisha vifo.
Husababisha ongezeko la umaskini.
Huathiri misingi ya utawala bora, demokrasia na utawala wa sheria.

WAJIBU WA VIJANA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSWA
Kila mtanzania anao wajibu wa kupambana na rushwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 26, 27 na 28... “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano” - Ibara ya 26 (1)...” Watu wote wanatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na unadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ta taifa lao” -Ibara ya 27 (2). Vilevile Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 39 kinatamka bayana kwa kila mtu mwenye taarifa kuhusu kufanyika kwa vitendo vya rushwa unaopangwa na mtu au kundi la watu anawajibika kutoa taarifa kwa TAKUKURU. Hivyo katika mapambano dhidi ya rushwa vijana wanapaswa kutekeleza mambo yafuatayo:-

1. Wawe mfano wa kuigwa kwa kutekeleza yafuatayo:-
Kutoshawishi, kutoa au kupokea rushwa ili kupata au kutoa huduma kwa wanajamii au vijana wengine.
Kataa na kukemea rushwa kila inapojitokeza.
Kuwaelimisha wanafunzi, vijana na jamii kwa ujumla juu ya rushwa na hasa madhara yake, haki na wajibu wao kwa njia ya nyimbo, ngonjera, mashairi, maigizo na sanaa mbalimbali. Wanajamii wengine hujihusisha na rushwa kwa kukosa ufahamu.
Kuelimisha jamii faida za kupambana na rushwa kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Kujifunza kwa bidii na kuwajibika ipasavyo kwa muda unaostahili kwanii uzembe huzaa vishawishi vya rushwa.
Kutoa ushirikiano wa dhati kwa TAKUKURU na vyombo vingine pindi unapohitajika. Kwa mfano kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa vinavyotendeka katika jamii.

2. Wawe jasiri kwa:-
Kukemea vitendo vya rushwa na kuwafichua wale wote wanaoshiriki kufanya vitendo vya rushwa.
Kufichua mianya inayotumiwa na wala rushwa ili iweze kuzibwa.

3. Wawe wazalendo kwa:-
Kufuata sheria, kanuni na taratibu za serikali.
Kutoshawishi, kutoa au kupokea rushwa ili kupata au kutoa huduma kwa wanajamii au vijana wengine.
Kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili kwenye kamati ya maadili ya mtumishi husika.

Chanzo cha habari: Takukuru

1 comment: