Wednesday, September 29, 2010

VIJANA WA TANZANIA NA SHILIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI

Vijana wengi ukiwaambia watoe maoni yao kuhusu shirikisho la Afrika Mashariki, hulikosoa shirikisho hilo kwa nguvu ao zote. Wamekuwa na hofu juu ya ushindani mkubwa wa ajira na bidhaa wanazozalisha. Wengi wametoa maoni kwamba shirikisho lisilishwe ili wawe na uwezo wa kushindana na nchi nyingine wanachama.

Lakini hiyo ni hofu tu, vijana wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu shirkisho la Afrika Mashariki, na wengi wamekuwa wakisubiri kuletewa taarifa na fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo badala ya wao kutafuta taarifa na fursa zaidi walizo nazo.

Vijana tumekuwa tulitazama shirikisho kwa macho mawili ya kawaida hivyo tunaona matatizo mengi ndani yake. Tumeshindwa kutumia jicho la tatu kuona fursa tulizonazo sisi kama vijana wa kitanzania. Vijana wenzetu wa nchi nyingine hutafuta taarifa na fursa ndio maana tunaona wanafanikiwa na kufaidika katika shirikisho la Afrika Mashariki. Sifa kubwa ya kijana mjasiriamali ni kuona fursa wakati wengine wanaona tatizo, na fursa yoyote ile lazima iwe na changamoto zake. Changamoto huwa hatuzikimbii bali hinakabiliana nazo ili tupate matokeo mazuri.

Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya, Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo na kuweza kuwa mzalishaji na mlishaji wa Jumuiya Je, hiyo siyo fursa kwa kijana? Nchi zote haziwezi kuwa sawa kwa kila kitu kuna vitu ambavyo wenzetu wametuzidi na kuwa mambo mengi ambayo na sisi tumewazidi. Hamna sababu ya kupinga shirikisho wala kuomba muda mwingi zaidi wa kujiandaa. Kwani hata timu ya mpira ikijiandaa kwa muda mrefu bado itakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao, mbinu kabambe zinahitajika wakati wa mchezo.

Vijana tukumbuke kwamba sasa tupo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo tutambue changamoto zinazotukabili na kutafuta mbinu za kupambana na changamoto hizo. Vile kujifunza, kujikosoa na kuiga kile kilicho bora kutoka kwa wenzetu ambao tunaona wepiga hatua mbele. Hamna haja ya vijana kukaa na kupoteza muda kwa kupinga uwepo wa Jumuiya hii.

Ushiriki wa vijana wa Tanzania katika shughuli za mtangamano unawawezesha vijana kulinda maslahi ya Tanzania, na kufaidika na fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vijana wanatakiwa kutafuta taarifa mbalimbali zinazohusu Jumuiya ili kupanua elimu waliyonayo kuhusu mtangamano wa Afrika ya Mashariki ikiwa pamoja na fursa zilizopo na jinsi ya kuzihimiza, lakini pia kuhusu changamoto zilizopo na jinsi ya kukabiliana nazo. Vijana tujiunge katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili kwa pamoja tuwezekushindana kikamilifu wa wafanyabiashara qa nchi nyingibe. Umakini, uhalali na ubora wa shughuli ambazo zifanywa na vijana wajasiriamali ni muhimu katika kuimili ushindani huo. Bidhaa zote tunazozalisha ni muhimu kuhakikisha bidhaa hizo zina ubora unaokidhi mahitaji ya soko ili kuvutia mlaji.

Yafuatayo ni maeneo ya msingi yanayohusishwa katika soko la pamoja, ambayo ni:-
a)Soko la uhakika kwa bidhaa mbalimbali, zikiwemo bidhaa za kilimo na viwanda katika jumuiya;
b)Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kusafiri katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya(Free Movement of people)
c)Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya kazi katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya (Free Movement of workers);
d)Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya biashara ya kudumu katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya (Free Movement of servies); utekelezaji wa hatua hii unawahakikishia uhuru wa soko la biashara ya huduma katika sekta zilizofunguliwa na nchi wanachama kwa kuondoa vikwazo hatua kwa hatua, na kutoanzisha vikwazo vipya.
e)Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kuwekeza mitaji katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya (Free Movement of Capital); utekelezaji wa hatua hii utawezesha kuondoa vikwazo kwa raia wa Afrika Mashariki kuwekeza kwenye soko la mitaji katika nchi nyingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hatua kwa hatua kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji;
f)Haki ya raia wa Afrika Mashariki kuanzisha na kuendesha shughuli za biashara na uchumi katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya (Right of Establishment); utekelezaji wa hatua hii unawahakikishia raia wa Afrika Mashariki haki ya kuanzisha na kuendesha shughuli za biashara na kiuchumi katika nchi yoyote Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bila ubaguzi kwa misingi ya utaifa au taratibu za uanzishaji kampuni hatua kwa hatua.
g)Aidha, Nchi wanachama zimekubaliana kuanzisha sheria na maeneo yanayolindwa kwa wananchi wa nchi husika na kuyawasilisha katika Baraza la mawaziri la jumuiya ya Afrika Mashariki ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya itifaki ya soko la pamoja kupata nguvu ya kisheria kwa lengo la kukubaliana jinsi ya kufungua maeneo hayo katika siku za usoni.
h)Haki ya ukazi kwa raia wa Afrika Mashariki katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya (Right of Residence); utekelezaji wa haki hii unawawezesha raia wa nchi wanachama watakaopata ajira au kuanzisha shughuli za kiuchumi kuishi katika nchi yoyote mwanchama, kulingana na taratibu zilizokubalika.

Dira kuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kukuza kipato, kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki, kukuza uchumi, na kujenga ushindani wa kanda katika ngazi ya kinataifa. Katika kutekeleza azma hii, nchi wanachama zinanufaika kutokana na mahusiano mazuri ya kibiashara na uwekezaji. Aidha nchi wanachama zinanufaika na progran kuendeleza mitandao ya barabara, reli, umeme, elimu, afya, usalama na utawala bora.

Kwa ujumla dira, malengo na mikakati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni nzuri endapo itafikiwa kwa wakati na walengwa kunufaika. Utekelezaji unahitaji uwajibikaji mkubwa wa Jumuiya serikari ya nchi husika na wananchi wake. Vijana wananafasi kubwa katika kutimiza malengo ya Juimuiya. Hivyo kila kijana anatakiwa atambue fursa na wajibu alionao katika jumuiya ili kuinua uchumi wake binafsi na wa Taifa kwa ujumla.

Na,
Innocent Mbele
Mwenyekiti mtendaji, FASO

No comments:

Post a Comment