RAIS Jakaya Kikwete amewataka wahisani kuendelea kusaidia sekta ya kilimo nchini ili kufikia asilimia 10 ya pato la taifa.Alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa Mpango wa Uwekezaji katika Kilimo na Uhakika wa Chakula (TAFSIP) wa mwaka 2011/12 mpaka 2020/2021.
Rais Kikwete alisema kilimo kitafanikiwa kutokana na misaada ya wahisani hao, sekta binafsi na vyama vya kijamii vinapaswa kusaidia sekta ili kufikia malengo yake.
"Malengo ni kufikia asilimia 10, sasa tuko kwenye asilimia 4, hivyo pato la taifa likifikia asilimia 10, tutakuwa tumefika mbali,"alisema Rais Kikwete.
Alisema endapo mpango huo utafanikiwa, wakulima wengi nchini wataondokana na umasikini na uchumi wan chi kukua.
"Uchumi wetu unakuwa vizuri na sasa umekua kwa asilimia 7 hivyo kama tutafanikiwa kukuza kilimo na kufikia asilimia 10 ya pato la taifa, basi nao uchumi utafikia asilimia 10 katika sekta zote.
"Kilimo ndicho kinachotoa chakula na pia kinaingiza fedha za kigeni.
"Japokuwa hakijakuwa kama tulivyotegemea, nia hasa ni kuhakikisha kilimo kinakuwa,"alisema.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania ili sekta ya kilimo ikue kwa kasi na kuwapo kwa uhakika wa chakula nchini.
"Tutasaidia mpango huo ambao unatekelezwa pande zote mbili za Tanzania Bara na Visiwani,"alisema Balozi Lenhardt.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment