Alizeti haitoi
mailisho pekee, pia inatoa mafuta bora kwa afya ya binadamu na pia
malighafi inayotumiwa na nyuki kutengeneza asali.
Unapotengeneza chakula cha mifugo peke
yako, si tu kupunguza gharama, lakini pia inakupa uhakika wa kuwa na
chakula bora. Pia Wafugaji wa nyuki wanaopanda alizeti wanapata faida ya
ziada kwa kupata asali iliyo bora kwa sababu nyuki hukusanya poleni
kutoka kwenye alizeti wanapofanya ushavushaji.
Chanzo kizuri cha protini
Chakula cha mifugo kinachotengenezwa
kutokana na alizeti ni chanzo kizuri cha protini kwa ajili ya mifugo,
hasa ng’ombe wa maziwa, kuku, nguruwe na hata sungura. Malisho haya yana
kiasi kikubwa cha protini, nyuzi nyuzi na kiasi kikubwa cha mafuta.
Malisho haya yana protini kiasi cha asilimia 29-30, kiasi cha nyuzi
nyuzi asilimia 27-31.
Moja ya tabia nzuri ya alizeti ni
kwamba haina vitu vinavyoathiri virutubisho kwa mifugo, hata hivyo, ina
kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi na mashudu yake kuwa magumu kiasi, jambo
ambalo husababisha ugumu kidogo kwenye kusagwa tumboni. Mbali na
virutubisho vya aina nyingine, alizeti ni chanzo kizuri cha kalishamu,
fosiforasi na vitamini B.
Ubora wa alizeti inayotumika kwa
ajili ya malisho ya mifugo inategemeana na namna ambayo imetayarishwa.
Kwa mfano, alizeti inayosagwa bila kuondoa maganda ya nje, ina kiasi
kikubwa cha nyuzi nyuzi (kati ya asilimia 27-30, lakini inakuwa na kiasi
kidogo cha protini asilimia 23). Alizeti ambayo imetayarishwa kwa ubora
wa hali ya juu huwa maganda yameondolewa na inakuwa na kiasi kikubwa
cha protini, kiasi cha asilimia 40.
Mkulima anapaswa kufahamu kuwa alizeti
bado inakuwa na virutubisho hata kama haitatayarishwa kwa ustadi.
Mfugaji anaweza kutumia soya na karanga badala ya alizeti, lakini ni
lazima apeleke alizeti kupima kuhakikisha kuwa ina nyuzinyuzi na
virutubisho kwa kiwango cha nyuzinyuzi na protini kinachokubalika.
Inapendekezwa kutumia alizeti
Kulingana na utafiti ambao umefanyika
nchini Tanzania, alizeti iliyochanganywa na pumba ya mahindi kwa kiasi
cha asilimia 30, kisha kulishwa ng’ombe aina ya Zebu ina uwezo wa
kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 6.6 kwa siku mpaka lita 8.1
kwa siku. Nchini Zimbabwe, mashudu ya alizetu huchanganywa na mahindi
pamoja na mabua ya mahindi ambayo yamewekwa urea kwa kiwango cha
wastani wa kilo 4.4 kwa siku, na kulishwa ng’ombe aina ya Jersey pamoja
na ng’ombe chotara ambao hulishwa katika machungo ya wazi, Ng’ombe hawa
huongeza kiasi cha maziwa kwa wastani wa kilo 5.8 mpaka kilo 6 kwa siku.
Aina ya alizeti
Kuna aina mbili za alizeti, alizeti fupi
na alizeti ndefu. Aina ndefu hurefuka mpaka kufikia kiasi cha urefu wa
mita 1.5-2.4. Uzalishaji wake ni hafifu ukilinganisha na mbegu za
kisasa. Aina hii mara nyingi huwa ile inayojulikana kama Hungary nyeupe
na Fedha. Alizeti fupi ni inayotokana na mbegu za kisasa ambayo huwa na
urefu wa mita 1.2, aina hii huwa na mavuno mazuri zaidi ukilinganisha na
aina ndefu.
Kutengeneza chakula cha mifugo
Kilo tatu na nusu za alizeti inapokamuliwa hutoa mafuta lita moja na mashudu kilo mbili na nusu.
Resheni kwa ng’ombe wa maziwa
•Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi ili kutengeneza chakula cha ng’ombe.
•Mlishe ng’ombe anaezalisha maziwa kwa
wingi kiasi cha kilo 4 ya mchanganyiko huo na kilo 2 kwa ng’ombe
anaezalisha kiasi kidogo cha maziwa.
•Mbali na kulisha mchanganyiko huo,
ng’ombe wa maziwa ni lazima apewe kiasi kingine cha chakula cha kawaida
cha kila siku kama vile matete, hay, au aina nyingine yoyote ya malisho
bora kwa kiasi cha kutosha.
Resheni kwa ajili ya kuku
Chakula cha kuanzia:
Changanya kilo 22 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi
Chakula cha kukuzia: Changanya kilo 20 za mashudu ya alizeti na kilo 100
za pumba ya mahindi au chenga.
Chakula kwa ajili ya kuku wanaotaga: Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za chenga za mahindi
ZINGATIA:
Unapotengeneza chakula kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa, mfugaji ni lazima
ahakikishe kuwa mashudu hayazidi asilimia 20 ya resheni ya kulishia.
Kwa ajili ya kulishia kuku, alizeti isizidi asilimia 7 ya jumla ya
resheni.
Namna ya kuzalisha alizeti
Hali
ya hewa: Alizeti hustawi vizuri zaidi kwenye udongo tifutifu, wenye
rutuba ya kutosha. Zao hili lina mizizi inayoenda chini kwa kiwango cha
kikubwa hivyo kuiwezesha kustawi hata katika sehemu yenye kiwango kidogo
cha mvua. Kiasi cha wastani wa milimita 500-750 za mvua zinatosha
kabisa kwa uzalishaji wa alizeti. Inaweza kulimwa kutoka usawa wabahari
mpaka kufikia mwinuko wa mita 2600 kutoka usawa wa bahari.
Maandalizi ya shamba
Ni lazima kuhakikisha kuwa shamba limelimwa vizuri, ili kuweza kupata sehemu nzuri ya kusia mbegu.
Nafasi: Mbegu zinaweza
kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30 kwa kiasi cha kilo 2 kwa
ekari moja (sawa na kilo 5 kwa hekari). Panda mbegu 3 kwa kila shimo,
kisha acha mmea mmoja kwa kila shimo mimea inapofikia urefu wa sentimita
10-20.
Matumizi ya Mbolea
Alizeti hufanya vizuri kwenye udongo
wenye rutuba. Matumizi ya mbolea inayotokana na miamba aina ya fosifeti
inafaa zaidi kwa kuwa alizeti inahitaji fosifeti kwa kiasi kikubwa.
Matumizi ya mbolea mboji iliyoandaliwa vizuri itaongeza virutubisho vya
ziada kwenye udongo.
Alizeti hukua vizuri katika sehemu isiyokuwa na magugu. Palilia alizeti inapokuwa na urefu wa mita 0.7 (Kiasi cha wiki 4).
Ndege waharibifu
Ndege wanaweza kuharibu kiasi cha
asilimia 50 ya alizeti endapo hawatafukuzwa. Ili kuzuia uharibifu huo,
mkulima anaweza kuchukua hatua zifuatazo;
•Vunja shina la alizeti kufikia usawa wa
magoti kabla ya alizeti kukauka. Unaweza pia kuvunja katika urefu
wowote lakini alizeti iangalie chini ili kuzui ndege kudonoa.
• Ondoa alizeti shambani baada ya kukauka na kuihifadhi.
• Ubanguaji unaweza kufanyikia nyumbani kwa kutumia fimbo
• Alizeti ni lazima ikaushwe mpaka kufikia kiwango cha unyevu wa asilimia 10 kabla ya kuhifadhiwa
Chanzo:mkulima mbunifu,