Monday, April 16, 2012

UTUPA, MMEA WA AJABU UNAOUA WADUDU

Utupa (Tephrosia vogelii) ni mmea wa jamii ya mikunde ambao huishi kwa muda unaozidi miaka mitatu. Mmea huu hutoa maua mengi, kuzaa mbegu nyingi na una majani mengi. Mmea huu hukua haraka pia ni rahisi kuzalisha. Huweza kukua hadi kufikia urefu wa futi 10. Inashauriwa kuukata baada ya miaka mitatu ili kurefusha maisha yake na kuwezesha kutoa majani mengi. Mmea huu hustawi vizuri sehemu mbalimbali na zipo aina kuu tatu. Aina hizo zinatofautishwa kwa maua yake kama ifuatavyo: inayotoa maua ya njano, pinki na meupe.

Utupa unaoteshwa kwa mbegu na unakuwa tayari kutumika baada ya miezi 4-6 tangu mbegu zipandwe. Sehemu yenye sumu katika utupa ni majani na mizizi. Inadhuru visumbufu wa mimea vinapokula na kugusa, hii inavisababishia kukosa hamu ya kula.

Utupa unaweza kutumika kama kiuatilifu cha wadudu kama vile kupe, utitiri, kimamba, cabbage headworm, viwavi, sota funza wa vitumba, bungua wa mahindi, vithiripi, fuko, viroboto, chawa na magonjwa ya ngozi.

Pia utupa unafaa kutandaza shambani na kurutubisha ardhi.
Kutayarisha dawa ya majani ya utupa Kwa ajili ya kuua wadudu

Chuma majani mabichi kulingana na mahitaji ya shamba lako (hasa kabla mmea haujatoa mbegu kwani wakati huo dawa aina ya tephrosine ipo nyingi zaidi).

Yatwange mpaka yawe laini.

Loweka katika lita 20 za maji safi kwa muda wa masaa ishirini na nne katika uwiano wa 1:20 (kg 1 ya utupa kwenye lita 20 za maji).

Chuja mchanganyiko huo vizuri ili kuondoa vipande vya majani. Unaweza kutumia chujio la bomba.

Nyunyizia mboga zako au mimea mingine kama dawa nyingine. Tofauti iliyopo kati ya dawa hii na madawa ya kemikali ni kwamba haina harufu kali na madhara kwa afya ya mnyunyiziaji.

Dawa hii huweza kuua viwavi wa nyanya, nondo wa kabeji, wadudu mafuta na funza wa mabua ya mahindi (stalk borers), wadudu wanaoshambulia matango na kahawa.

Inapendekezwa itumike kabla mimea haijashambuliwa. Huua pia wadudu walao majani na mashina kama viwavi jeshi.

Unga unaotokana na majani ya utupa unaweza pia kutumika kuhifadhi nafaka hasa kwa ajili ya mbegu.
Kutayarisha dawa ya unga wa utupa

Twanga majani hadi yawe laini na uanike.

Saga majani yaliyotwangwa na kuanikwa kuwa unga.

Wakati wa kuotesha mazao, changanya unga wa dawa na mbegu ya zao unalotaka kupanda.

Tumia shambani kwa kunyunyizia dawa kwa kushika kwenye vidole vitatu kwa shina moja la kabichi.
Matumizi ya ghalani

Majani ya utupa yanatumika pia kuhifadhia mazao ghalani.

Yanatumika kufukuza fukuzi na mende wa maharage.

Chuma majani ya utupa, anika kwenye kivuli, twanga majani kupata unga.

Pima na changanya gm 100 katika kg 100 za nafaka/mikunde.

Dawa hii inatumika pia kuhifadhi mahindi.
Tahadhari kwa watumiaji

Kuvaa kinga ya mwili mzima wakati wa unyunyuziaji

Tumia dawa baada ya uchunguzi wa visumbufu

Usile mazao kabla ya siku 10- 14 kwisha baada ya kunyunyuzia dawa

Iwekwe mbali na watoto, maji na mifugo

Utupa ni sumu kali kwa samaki, inaweza kuua wadudu marafiki na wanyama.

Kwa nafaka za chakula hakikisha unga wa dawa unakaushwa vya kutosha kwani unaweza kusababisha harufu kali kwenye nafaka.

No comments:

Post a Comment