Monday, April 16, 2012

16th April 2012

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (Mviwata) umeandaa kongamano la kitaifa ambalo pamoja na mambo mengine litajadili na kutoa tamko la kupinga mauaji ya wakulima wadogo nchini, wanaouawa katika harakati za kutetea ardhi yao.

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mjini Morogoro kesho ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya siku ya Wakulima Wadogo Ulimwenguni, litajadili athari za uporaji wa ardhi kwa wazalishaji wadogo nchini.

Aprili 17 kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya harakati za wakulima wadogo ulimwenguni. Maadhimisho hayo hufanyika ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya wakulima wadogo 19 yaliyotokea nchini Brazil mwaka 1996 wakiwa katika harakati za kutetea haki yao na kuzuia uporaji wa ardhi waliyokuwa wakiitegemea kwa uzalishaji.

Mratibu wa maandalizi ya kongamano hilo, Thomas Laiser, alisema jana kuwa Mviwata imeandaa kongamano hilo ili kuzungumzia mustakabali wa wakulima wadogo Tanzania, ikiwemo mauaji ya wakulima yanayoendelea kutokea wakati wa harakati za kuwaondoa kwenye maeneo yao.

“Katika miaka ya karibuni nchini Tanzania tumeshuhudia kasi ya uporaji wa ardhi ya wazalishaji wadogo vijijini ikijumuisha matumizi ya nguvu kupita kiasi na hata mauaji jambo ambalo halitoi ishara njema ya hatma ya wakulima na wazalishaji wengine wadogo,” alisema Laiser ambaye pia ni Afisa Ushawishi na Utetezi wa mtandao huo.

Aliongeza kuwa “uhamishwaji kwa nguvu ili kupisha wawekezaji wa ndani na nje na wakati mwingine upanuzi wa ardhi za hifadhi, zimetajwa kuwa sababu za kuhalalisha vitendo hivyo ambavyo vimewaacha wazalishaji wengi wadogo katika baadhi ya maeneo wakiwa wamepoteza makazi, mali na maisha yao.”

Laiser alitolea mfano wa matukio ya kuwahamishwa kwa nguvu wafugaji katika bonde la Ihefu, hifadhi ya Loliondo, Malinyi Ulanga, Meatu, Kiteto na kwingineko nchini yakiwemo mauaji ya wakulima watano wilayani Ulanga siku za karibuni ni mfano wa adha ambazo wazalishaji wadogo wamekuwa wakikabiliana nazo kutokana na uporaji wa ardhi unaoendelea kufanyika.

Kongamano hilo pia litazijadili athari mahsusi zinazowakabili wanawake na watoto vijijini katika harakati za utwaaji ardhi na kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa na serikali wa ngazi mbalimbali kuwalinda na kuisimamia haki ya ardhi ya wazalishaji wadogo vijijini.

Laiser alisema kongamano hilo litakuwa na washiriki zaidi ya 90 wakiwemo wakulima 70 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kati yao theluthi mbili wakiwa ni wanawake.

Washiriki wengine kwenye kongamano hilo watakuwa ni wanahabari, waalikwa toka mashirika yanayotetea haki za ardhi nchini, wawakilishi wa taasisi zingine za kiraia, wanaharakati, wanataaluma na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa mtandao huo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment