UNAPOFANYABIASHARA kuna baadhi ya biashara zitafanikiwa kupitia biashara yako, na zingine zitashindwa kufanikiwa kwa sababu ya biashara yako. Zifuatazo ni mbinu sita muhimu sana kuzingatia uanzishapo au kuendeleza biashara yenye mafanikio.
Je biashara yako inafaida endelevu?
Faida ndogo ni hatari kwa ustawi na uendelevu wa biashara. Fikiria unapata asilimia 2 kama faida halisi na endapo bei zikipanda kwa asilimia chache tu unakuwa katika hatari zaidi.
Faida kubwa inakupa nafasi ya kuhimili changamoto katika soko endapo gharama zikipanda, unakuwa na uwezo wa kuendelea kuuza bidhaa zako au kutoa huduma kwa bei ile ile, kwa maana hiyo utaendelea kubakia na wateja wako na wengi wapya watakuja kuliko ukiwa na faida ndogo na gharama zikipanda unahitaji pia kupandisha bei kitu kinachoweza kupunguza wateja na faida usiione kabisa.
Mifano ya faida kubwa tumeiona hapa nchini kuna baadhi ya makampuni makubwa na maarufu yanaweza kubaki na bei ile ile hata kwa miaka 3 mpaka 5 bila kujali upandaji wa gharama zingine kama kodi na usafirishaji.
Pato zuri kwa kila mauzo.
Hili hukosewa na wajasiriamali wengi, ni vigumu kufanikiwa ukiwa na bei ya chini sana. Fikiria unauza bidhaa kwa shilling 1,000 na unataka kufikisha mauzo ya millioni 10 ni lazima uuze bidhaa au huduma mara 10,000 lakini kama bei zako ni shilling 10,000 na unataka kufikisha mauzo ya million 10 ni lazima uuze bidhaa au huduma mara 1,000 tu. Fikiria wepesi uko wapi na kipi kinawezakana kutekelezeka kiurahisi kwa biashara ndogo na za kati.
Upekee wa bidhaa au huduma.
Wajasiriamali tunashauriwa kuwa wabunifu na kuacha kuiga mambo ya wengine. Nchi za wenzetu wanaendelea kwa kuwa na biashara nyingi mpya zilizobuniwa kuliko za kuiga, nasi hatupigi hatua sana kwa kuwa tunaiga mno.
Upekee wa bidhaa au huduma unakupa nafasi kubwa ya kuthibiti soko kwani inakuwa ngumu kwa mtu mwingine kuanzisha. Mathalani tunashuhudia tasnia ya muziki na filamu nchini wanapigania haki miliki, hii ni njia moja wapo kama umebuni bidhaa au huduma yako unalindwa kisheria na ni ngumu mtu mwingine kuiga bila makubaliano nawe. Hivyo ni wito pia kwa wajasiriamali mnaogundua au kubuni bidhaa au huduma mpya kuangalia namna gani sheria za kibisahara zitalinda ugunduzi wako na kukupa faida zaidi.
Fanya kitu ukipendacho
Ni vigumu sana kufanya kitu bila ari. Chagua biashara inayoendana na kitu au fani uipendayo. Usiingie kwenye biashara kwa kuona tu takwimu zinaonesha faida kubwa. Kumbuka mafanikio kibiashara hayaji kwa siku chache bali huweza kuchukua hata miaka. Biashara ni maisha, hivyo fanya biashara uipendayo na utakayoifanya kwa muda mrefu wa maisha yako.
Angali mfano wa matajiri wengi nchini biashara zao aidha ni za urithi tokea enzi za mababu au wameanzisha wenyewe lakini wamedumu nazo kwa miaka mingi sana. Vile vile nitoe rai kwa wazazi tusiwashinikize vijana wetu kufanya biashara yoyote kisa kakataa masomo na pesa ipo. Wazazi wengi wamepoteza fedha mtindo huu. Mdadisi mwanao anapenda nini, kama huna muda siku hizi kuna watalaam washauri wa biashara, mpeleke apate ushauri/elimu ya saikolojia, ujasiriamali na biashara, baada ya hapo atafanya biashara yenye tija na mafanikio.
Je biashara itakupa mtiririko mzuri wa fedha?
Ni dhahili biashara inaweza kuonekana inafanya vizuri kimauzo na faida lakini huoni mtiririko wa fedha. Fedha inahitajika kulipia ankara na matumizi mengine ya biashara. Kama biashara ina mauzo mazuri lakini haina fedha ni ngumu kukua. Ni vyema kila mara kufanya makisio ya fedha zinazohitajika kuendesha shughuli za biashara za kila siku.
Je ni fulsa zipi zakukuza biashara yako? Wajasiriamali wengi tunapenda na kufurahia kuona biashara inaleta fedha, lakini inapoleta hasara tunagadhabika. Ni vizuri kuwa na mikakati ya namna gani biashara yako itakua kuliko kuiacha kuendeshwe na matukio.
Wajasiriamali wengi wanapoteza fursa za kukua kibiashara kutokana na mapungufu katika mipango ya ukuaji.
Mathalani faida imepatikana ya kutosha lakini eneo na mazingira ya biashara hayaruhusu kupanua biashara, ni bora ufungue nyingine na nyingine na nyingine kuliko kufurahia fedha nyingi zilizokaa bure katika akaunti yako benki.
Jifunze kuthubutu, kuamini watu na fanya kazi na watu kwani watu ndio watakupa mafanikio. (mwananchi,25/08/2011)
No comments:
Post a Comment