Thursday, May 9, 2013

UFUGAJI WA NGURUWE

Photo: Pig peering over a wall
“Ufugaji wa Nguruwe ni lazima uwe wa kisasa ili kupata mazao bora. Unaweza kupata kila unachohitaji wewe, familia na hata ndugu zako kutokana na ufugaji wa nguruwe”, anasema Bwana Lomaiyani Molel kutoka Arusha. Jamii nyingi hapa Tanzania huchukulia nguruwe kama mnyama mchafu na asiyefaa kuwa karibu naye na hata kwa matumizi kama lishe. Zaidi, nyama yake inapendwa na haina madhara kwa afya na inapendekezwa kuliwa zaidi kuliko nyama nyekundu. Unaweza kuanzisha mradi wa nguruwe kwa gharama ndogo lakini baada ya kipindi cha miezi tisa tu ukaanza kujipatia kipato kutokana na ufugaji huo.


Ufugaji
Kwa kawaida nguruwe wanafugwa na watu wa kada zote, wafugaji wadogo wadogo na hata wakubwa. Aina hii ya ufugaji huweza kumpatia mkulima kipato pamoja na lishe kwa familia, na hauhitaji gharama kubwa.

Banda

Nguruwe wanahitaji kuwa na banda lililojengwa kwa vifaa nafuu. Unaweza kutumia mchanga na simenti kuweka sakafu, ama ukatumia udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kuweka sakafu. Ukubwa wa banda unategemeana na idadi ya nguruwe unaotaka kufuga. Mita 3 kwa mita 2.5 zitawaweka guruwe 8-10 wanaonenepeshwa kwa soko au nguruwe jike mmoja na nguruwe dume mmoja.

Malisho

Ulishaji wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula kulingana na mazingira wanayofugwa. Unaweza kuwalisha kwa kutumia majani laini ya aina mbalimbali, na pia hulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka (pumba). Unaweza kuwalisha kwa kutumia mashudu au pumba aina ya Wheat Poland. Pia unaweza kuwalisha kwa kutumia mabaki ya jikoni.

Kuzaliana


Nguruwe hubeba mimba kwa kipindi cha siku 114, ambazo hugawanyika kwa miezi 3, wiki 3 na siku 3. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kuzaa watoto 6 hadi 14 kwa mara moja. Watoto wa nguruwe (piglets) huanza kula chakula cha kawaida wanapofika umri wa mwezi mmoja na nusu mpaka miezi miwili. Endapo nguruwe watapata matunzo mazuri, baada ya miezi 8 wanakuwa na uzito kati ya kilo 50-70 na wanaweza kuuzwa.
 
Matunzo

Baada ya nguruwe kuzaa anatakiwa kupatiwa chakula cha kutosha na cha kutia nguvu ili kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wake. Watoto wa nguruwe wachomwe sindano ya madini ya chuma (Iron injection) baada ya siku moja au mbili toka kuzaliwa. Hii ni muhimu sana vinginevyo wanaweza kufa wote. Kata meno (tooth clipping) baada ya miezi mitatu. Unaweza kuhasi madume (castration) baada ya miezi miwili.


Magonjwa yanayoathiri nguruwe

Kuna aina nyingi za magonjwa yanayoshambulia nguruwe, lakini yapo yale yaliyozoeleka ambapo ni lazima kukabiliana nayo ili kuwa na ufugaji wenye tija.


Ugonjwa wa miguu na midomo

Ugonjwa huu huathiri nguruwe sehemu za miguu na midomo. Ni ugonjwa ambao hushambulia nguruwe mara kwa mara hasa wasipokuwa na matunzo mazuri. Ugonjwa wa miguu na midomo, hudhoofisha nguruwe kwa haraka sana, ikiwa ni pamoja na kupungua uzito.



Chanjo:
Chanjo kwa ajili ya ugonjwa wa midomo na miguu (FMD vaccine) hutolewa kila baada ya mwaka mmoja. Hii inasaidia kuwaweka nguruwe wako katika hali nzuri zaidi bila kushambuliwa na magonjwa hayo.


Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba halisi. Inapotokea nguruwe wakawa wameshambuliwa kinachofanyika ni kutibu magonjwa nyemelezi kwa kutumia antibiotics.
Homa ya Nguruwe (Swine fever)

Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe huenea kwa haraka sana miongoni mwa makundi ya nguruwe, na huua kwa haraka sana, lakini hauna madhara kwa binadamu na hauambukizwi kwa binadamu. Nguruwe walioambukizwa waanshikwa na vindonda ama mapunye kwenye ngozi. Pia masikio na ngozi huwa mekundu.

Chanjo: Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba. Kinachofanyika mlipuko unapotokea ili kuwa salama ni kuwateketeza nguruwe wote walioathirika na kuanza upya. Unaweza kuteketeza kwa kuwachoma moto.

Muhimu: Baada ya kuwateketeza nguruwe wagonjwa, safisha banda kisha nyunyiza dawa aiana ya Acon au Ectomin, na uache banda wazi kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kuweka nguruwe wengine.
Ugonjwa wa mapafu (Pneumonia)


Huu ni ugonjwa unaoshambulia sehemu za koo na mapafu ya nguruwe, ambapo husababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria (Secondary bacterial), joto kupita kiasi, vumbi na gesi inayotokana na madawa makali.



Tiba:
Homa ya mapafu kwa nguruwe inatibika kwa kutumia antibiotics. Pamoja na kuwaweka wanyama sehemu safi, isiyo na baridi kali au joto la kupitiliza kiwango.

Kimeta (Anthrax)


Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Bacillus anthracis, wadudu hawa wanabaki kuwa hai kwa muda mrefu na wanaweza kuwa kwenye udongo wakiwa hai kwa kipindi cha miaka mingi.


Chanjo:
Chanja nguruwe wako dhidi ya kimeta kama utakavyoelekezwa na wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.

Tiba:
Unaweza kutibu nguruwe wako kwa kutumia dawa aina ya Penisilin au Oxytetracycline.

Muhimu:
Homa ya nguruwe ni lazima iwekewe karatini kwa sababu husambaa kwa haraka sana. Nchini Tanzania mlipuko wa homa ya nguruwe umekuwa ukitokea mara kwa mara maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na katika mkoa wa Mbeya.

Ufugaji wa nyuki ni kazi nzuri ya ziada

Ufugaji wa nyuki unaweza kuwa chanzo kizuri cha kipato cha ziada kwa wakulima wadogo wadogo.

Uzalishaji wa asali nchini Tanzania umekuwa ukitegemea sana wafugaji wadogo wadogo, wanaotumia njia za kiasili kama vile mizinga ya magogo au vyungu, kwa nyuki wa kiafrika ambao ni wengi sana kwenye mapori.


Ni muhimu kuwa na utaalamu wa kufuga nyuki


Mkulima ambae anahitaji kufuga nyuki ni lazima awe na uelewa wa mzunguko wa maisha ya nyuki. Anaye anza ni lazima aulize wafugaji wenzake ambao wana uzoefu wa kutosha, au kujiunga katika kikundi cha ufugaji ili apate ufahamu zaidi juu ya ufugaji wa nyuki.


Tafuta sehemu salama kwa ajili ya mzinga


Ni vizuri kutafuta mahali pazuri, salama, na penye sifa ya kufugia nyuki. Vifaa vyote vikishapatikana jambo linalofuata ni kuchagua mahali gani pa kuweka mzinga. Ni vizuri sehemu hii ikawa mahali ambapo makundi ya nyuki hukusanyika mara kwa mara.


Ni wapi pa kuweka mzinga!


Mara nyingine kupata eneo sahihi ni tatizo. Ni vizuri kuzingatia yafuatayo:


• Kulingana na hali ya kujilinda ya nyuki wa Afrika, haishauriwi kuweka mzinga shambani au karibu na shamba (weka umbali wa mita 150-200 kutoka kwenye mazao au nyumbani)
• Mzinga ni lazima uwekwe sehemu ambayo haitasababisha upotevu wa nyuki wanaporudi kutoka nje ya mzinga (wasiingie kwenye kundi lisilokuwa lao)
• Mizinga isiwekwe mbalimbali sana ili kuepusha usumbufu wa kutembea mbali kwa mfugaji wakati anapokagua. Eneo la kuweka mizinga ni lazima liwe :
• Kimya na mbali ya jumuia (hospitali, shule, na viwanja vya michezo) na maeneo ya biashara au viwanda.
• Karibu na maji masafi-kandokando ya mto, mabwawa ya samaki, mabeseni ya maji au sehemu ya matone.
• Iwe karibu na chakula cha nyukimimea inayochanua, miparachichi,
nazi, euculptus, migunga n.k
• Iwe sehemu ambayo ni kavu na isiwe sehemu ya tindiga kwani unyevu unyevu husababisha ugonjwa wa ukungu (fungal disease) na pia huzuia utengenezaji mzuri wa asali.
• Iwe mbali na watu waharibifu na iliyojificha kuepuka waharibifu.
• Sehemu ya mizinga ni lazima iwe inafikika kirahisi kwa kipindi chote cha mwaka ili iwe rahisi kuhamisha nyuki pale inapohitajika.
• Kuwe na kivuli cha kutosha hasa wakati wa mchana jua linapokuwa kali, na kusiwe na upepo mkali.
• Iwe mbali na mashamba, ambapo dawa za kuulia wadudu zinatumika.
Vichaka au wigo unaotenganisha mizinga na kuzuia wavamizi ni muhimu ili kupunguza ukali wa nyuki.


Jinsi ya kuweka mzinga


Baada ya sehemu ya kuweka mizinga kupatikana, kinachofuata ni kuandaa mizinga kwa ajili ya kuweka panapotakiwa.
• Safisha mzinga kuondoa uchafu wote, utando wa buibui na aina nyingine za wadudu.
• Weka chambo kwenye mzinga (waf ugaji wa nyuki mara nyingi hutumia nta) kwa kuipaka katika kuta za mzinga kwa ndani.
• Mzi nga unaweza kutundikwa kwenye mti, kwenye nguzo, kuweka kwenye jukwaa au kwenye miamba. Hii inategemea mkulima mwenyewe anapendelea njia ipi.


Aina za mizinga ya nyuki


Kifuniko juu (Top bar)


Hii ni aina ya mizinga inayotumika sana. Gharama yake ni karibi shilingi elfu hamsini za kitanzania. Ni aina nzuri sana kwa mtu anaeanza ufugaji wa nyuki kwa kuwa ni wa gharama nafuu. Hata hivyo mfugaji wa nyuki anaweza kutengeneza mzinga mwenyewe kama ana utaalamu wa useremala.


Faida


• Ni rahisi kukagua asali iliyo tayari.
• Ni rahisi kuvuna asali kuliko kuvuna toka kwenye mzinga wa kienyeji.
• Ni rahisi kuwatunza nyuki wakati wa kiangazi na inapokuwa hakuna maua. Mfugaji anaweza kuwapatia nyuki chakula ili kuongeza uzalishaji wa asali.
• Kurina asali ni rahisi sana ukilinganisha na mizinga ya magogo inayotundikwa juu ya mti, kwa kuwa haihitaji vifaa maalumu.
• Aina hii ya mizinga huwekwa kwa kuninginia jambo ambalo siyo rahisi kushambuliwa na wadudu/wanyama wanaokula asali. Inajaa haraka sana wakati ambao ni msimu wa asali kutengenezwa kwa wingi.


Hasara


• Kichane kwenye mzinga wa boksi hakina kishikizo hivyo huvunjika kwa urahisi sana kama hakitashikwa kwa uangalifu.
• Masega huvunwa pamoja na asali, jambo linalolazimu nyuki kutengeneza tena masega mengine na husababisha kupungua kwa uzalishaji wa asali.


Mzinga wa Langstroth unaweza kukupatia asali zaidi


Hii ni aina nzuri na rahisa sana ya mzinga. Pia hufahamika kama mzinga wa fremu, kwa kuwa ina fremu ambazo vichane vya masega hujishikiza. Pia una chumba kikubwa ambacho malkia hutagia mayai. Malkia anazuiliwa kuhama kwenda chumba kingine kwa kutumia waya. Kwenye chemba maalumu ya kutagia juu yake pana chemba ya kuhifadhia asali. Vichane vya masega vinatengezwa kwenye fremu na si kwenye nguzo kama ilivyo kwenye Top bar.
Ili kuvuna asali, mfugaji akiwa na masega yaliyojaa asali, hutumia vifaa maalum kwa ajili ya urinaji na kuhifadhi asali bila kupata tabu.


Langstroth ni gali kiasi fulani kwani huuzwa kuanzia kiasi cha TSh 70,000. Unaweza kuipata kutoka katika taasisi zilizopo hapo chini, taasisi na karakana binafsi, au wakala wa Serikali.
Chanzo: Mkulima Mbunifu

Nyanya zinahitaji matunzo ili upate mavuno

Mkulima atapata faida kubwa ikiwa atatunza zao la nyanya kwa uangalifu mkubwa.



Nyanya huzaa vizuri sana hasa zinapowekewa mbolea mboji au samadi iliyooza vizuri. Unaweza kuongeza mbolea ya minjingu kiasi cha kijiko kimoja cha chakula au vijiko 3 vya chai kwa kila shimo. Endapo ardhi ina upungufu wa mbolea asili, inashauriwa kupanda kwanza mimea yenye uwezo wa kutoa mbolea vunde bora kama vile kunde, mucuna, soya au clotalaria kabla ya kusia mbegu za nyanya au kupanda. Epuka mbolea za viwandani kwa kuwa nitrojeni ikizidi husababisha nyanya kuvimba, na baadaye kuoza kirahisi, pia husababisha mnyanya kukua kupita kawaida. Kuwa na nitrojeni iliyozidi kwenye udongo pia husababisha majani kuwa laini sana hivyo kuvutia wadudu na magonjwa kirahisi. Ushindani wa magugu dhidi ya nyanya zako unakuwa ni mkubwa sana, hasa sehemu zenye joto na unyevu mwingi.


Ili kudhibiti magugu kwenye eneo lililo wazi, fyeka mara kwa mara na uhakikishe kuwa ni mafupi kuliko nyanya mpaka hapo nyanya zitakapokomaa na kuiva. Acha magugu uliyofyeka kwenye shamba lako yawe kama matandazo ili kusaidia kupunguza au kuzuia mmomonyoko wa ardhi, kupunguza joto kwenye ardhi na kuhifadhi unyevu kwenye udongo. Hii inaweza pia kufanywa kwa kupalilia kwa mikono katikati ya mistari ya nyanya, na kuweka matandazo hayo katikati ya mistari.


Fito


Kwa aina ya nyanya zinazorefuka sana, chomeka walau fito zenye urefu wa mita 2 katika kila mche wa nyanya na ufungie kwa kutumia kamba. Badala yake unaweza kutengeneza kichanja chenye nyaya na nguzo kila baada ya mita 1 au 2 na nyingine yenye urefu wa mita 0.15 kutoka ardhini. Funga kamba imara kwa kila mnyanya. Mnyanya unaweza kuzungushwa kwa uangalifu mkubwa kwenye kamba hiyo kulingana na unavyokuwa.


Kukatia matawi ni muhimu sana kwa aina zote za nyanya. Unaweza kuacha shina kukua na kukata matawi mawili ya awali ili kuruhusu mmea kukua vizuri. Kata matawi kulingana na mmea unavyokuwa kwa wiki. Mmea unapokuwa na viriba 6 au 8 vya maua ni vizuri kukata kichwa ili kuwezesha ukuaji mzuri matunda yatakayotokea ambayo yatakuwa na soko zuri. Majani yaliyo karibu na ardhi ni lazima yaondolewe ili kusaidia kuzuia uwezekano wa mabaka kuingia kwenye mmea na matunda. Hakuna kanuni za kukata matawi au kupata idadi flani ya matunda kwa kila mmea, hii inategemeana na mkulima na aina ya nyanya.  Nyanya zinahitaji umwagiliaji mzuri katika siku za mwanzo toka kupandwa, wakati wa kuchanua, na wakati wa kukuza matunda. Kupatikana kwa maji ya kutosha kwenye minyanya, husaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na mazao na kukomaa kwa wakati mmoja.  Husaidia pia kupunguza uwezekano wa kuvimba na kuoza kwa nyanya, muonekano usiokuwa wa kawaida hutokana na ukosefu wa kalishamu ya kutosha wakati wa kutengeneza na kukuza matunda. Wakati wa kiangazi, ni muhimu kunyweshea angalau mara mbili kwa wiki. Unyeshaji kwa njia ya matone ni njia bora zaidi na isiyokuwa na madhara ukilinganisha na umwagiliaji wa mifereji, hii ni kwa sababu maji hudondoka kidogo kidogo kwenye shina.


Kuvuna


Nyanya kwa ajili ya kuuza zinaweza kuvunwa zikiwa bado na rangi ya kijani baada ya kukomaa, kisha zinaweza kuiva zikiwa zinasafirishwa kwenda sokoni, au zikahifadhiwa kwanza ili ziive. Nyanya zinazotumika kwa ajili ya kutengeneza supu, juisi, na mchuzi huachwa shambani mpaka ziive kiasi cha asilimia 85. Nyanya huchumwa zikiwa bado ngumu, lakini kiasi cha asilimia 65 huwa tayari kuchumwa kwa wakati mmoja.


Wadudu wa nyanya na njia za asili za kudhibiti


Sota (cutworms)


Hawa ni wadudu hatari wanaoshambulia vitalu vya nyanya. Wanakata shina la mimea iliyooteshwa au inayoota.


Ni nini cha kufanya;


• Ondoa magugu mapema, angalau wiki mbili kabla ya kupanda.
• Chimbua na utifue vizuri shamba lako kabla ya kupanda. Hii inasaidia kuwaibua sota na kufanya waliwe na maadui zao.
• Tengeneza wigo kulinda miche iliyohamishwa na kupandwa shambani. Wigo unaweza kutengenezwa kwa kuzungushia karatasi, karatasi ya foili, au ubao mwepesi kuzunguka sehemu ya bustani.
• Chimba karibu ya mimea iliyoharibiwa na uwateketeze sota.
• Wahifadhi wadudu wa asili wanaokula sota.


Vidukari (Aphids)



Vidukari hunyonya maji kwenye mimea na kusababisha mimea kupunguza uwezo wa kukua, pia hutoa ute kama asali, ambao husababisha unga unga unaosababisha mimea kukakamaa. Unga huu kwenye matunda husababisha yasipate soko.


Ni nini cha kufanya;


• Tunza wadudu wa asili wanaokula vidukari. Epuka kutumia madawa kwa wingi kwani yanaweza kuua wadudu wa asili wanaodhibiti vidukari.
• Tumia matandazo yanayong’aa. Vitu vinavyo akisi mwanga kama vile aluminiamu, husaidia vidukari wasiwezi kutua kwenye mimea.


Minyoo – (Root-knot nematodes)


Root knot huathiri sana nyanya.  Madhara yanakuwa makubwa zaidi sehemu yenye udongo wa kichanga na kunyeshea kwa kutuamisha maji. Minyoo husababisha vifundo kwenye mizizi. Mimea iliyoathiriwa hunyauka, na wakati mwingine hufa kabisa wakati wa jua.


Ni nini cha kufanya;


• Fanya mzunguko wa nyanya na nafaka.
• Usiweke kitalu cha miche mahali ambapo unahisi kuwepo magonjwa.
• Tumia aina ya nyanya inayostahimili magonjwa.
• Panda mazao mseto.
• Hakikisha kuna kiasi cha kutosha cha mbolea asili kwenye udongo.
Chanzo: Mkulima Mbunifu

Pandikiza parachichi upate mavuno zaidi

Msukumo wa uhitaji mkubwa wa parachichi kwa wingi na zenye ubora unawasukuma wakulima kutumia teknolojia mpya.



 
Upandikizaji hujumuisha aina mbili za mimea. Unachukua mmea mmoja ambao unadhani hauna tija nzuri, na sehemu ya mmea mwingine ambao una ubora zaidi na kupandikiza kwa kukata na kufunga pamoja ili kupata mbegu bora zaidi. Utaratibu wa kupandikiza hivi sasa umekuwa silaha ya wakulima kuwakomboa dhidi ya wadudu pamoja na magonjwa, na hili kwa sasa halifanyiki tena maabara kama ilivyokuwa awali na hii inadhibitishwa na yale tuliyojionea Njombe tulipotembelea wakulima.


 
Kwenye shamba la bwana Bosco Kidenya, ana kitalu chenye zaidi ya miche 1200 ya miparachichi, baadhi ikiwa tayari imeshapandikizwa na mingine ikiwa inasubiri kufikia wakati wa kupandikiza.  Huyu ni mmoja kati ya wakulima walio wengi wanaofanya kazi kwa karibu na CARITAS Njombe, kuboresha uzalishaji wa parachichi, pamoja na kuboresha kipato cha wakulima ambao wanazalisha matunda na mboga mboga.


Mbinu wanayotumia


Wakulima hukusanya kokwa za parachichi kutoka maeneo ya sokoni; wanachofanya ni kuhakikisha tu kuwa mbegu hiyo ni safi, haijaathiriwa na magonjwa na itaota. Baada ya hapo huchagua zile zenye muundo mzuri na kuzipanda kwenye boksi au kwenye sehemu ya kitalu. Baada ya kuota huziotesha kwenye makopo, au kwenye viriba kisha kuendelea kumwagilia maji mpaka zinapokuwa na umbo usawa wa penseli. Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati mmea umefikisha unene wa penseli. Kupandikiza kwa kutumia chipukizi lililolingana na mche unaopandikizia ni njia yenye mafanikio zaidi.


Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati ambao mizizi bado ni laini. Pandikizi litakalotumika wakati wa kupandikiza ni lazima lisiwe katika hatua ya ukuaji kwa wakati huo, na ni lazima umbo liwiane na mti linapopandikizwa kuzuia maji yasipotee na kusababisha pandikizi kukauka.


 
Mapandikizi ni lazima yatokane na aina ya parachichi ambazo zimeboreshwa kama vile hass, fuerte  au puebla. Kwa wale wakulima ambao mmea utatoa majani mapya. wana mkataba na Africado, watahitajikupata mapandikizi kutoka kwenye miti ya hass. Hii ina maanisha kuwa mkulima anayetaka kuanzisha kitalu kwa ajili ya kupandikiza ni lazima apande walau miti 5 ya parachichi aina ya hass ili kupata mapandikizi.


Njia ya kupandikiza ina ufanisi zaidi na ni rahisi kuliko kupanda miche upya, kwa kupandikiza inagharimu chini ya asilimia 75, kuliko kupanda miche upya na kuweza kupata aina ambayo inastahimili magonjwa. Wakulima pia wamekuwa na rikodi nzuri ya ongezeko la mavuno kutokana na mimea waliyopandikiza, pamoja na upungufu wa matumizi ya madawa.


Wakulima ambao wanafanya kazi zao chini ya CARITAS Njombe sasa wanaona faida kubwa inayotokana na kupandikiza, wameamua kuwekeza kwenye utaalamu huu na kuwa na miche mingi kwenye vitalu vyao. Hii ni mbinu ya kilimo ambayo ina faida kubwa kwa mkulima, huku akiwa amewekeza kwa kiasi kidogo sana katika kukabiliana na wadudu na magonjwa na kuepuka kuwa na mazao yenye ubora wa chini.



Namna ya kupanda


Nafasi halisi inayohitajika na mmea wa parachichi ili ukae vizuri ni nafasi ya 9m x 9m. Chimba shimo katika vipimo vya 60sm x 60sm kwa 60sm kwenda chini kisha tenga udongo wa juu na wa chini. Changanya udongo wa juu na mbolea ndoo moja iliyooza vizuri, pamoja na kiganja kilichojaa cha mbolea ya minjingu.


Ondoa mche wako kwenye kiriba ulipopandwa. Hii itakuwa rahisi zaidi endapo ulikuwa umenyweshea muda kidogo uliopita. Panda kwa kutumia udongo wa juu uliochanganya na mbolea na uweke mpaka kujaza shimo.


Mwagilia maji mara baada ya kupanda. Funika mmea mchanga kwa kutumia majani ya migomba au aina nyingine ya majani yanayofanana na hayo, mpaka kufikia kipindi ambacho mmea utatoa majani mapya.

Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai

Uelewa wa maisha ya mimea husaidia kwa kiasi kikubwa kwa hatua ya kuchukua kuilisha mimea hiyo.


 
Utunzaji wa udongo unategemeana kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kibiolojia. Kazi kubwa ya baadhi ya viumbe hai waliomo kwenye udongo, ni kumeng’enya mabaki ya mimea na viumbe hai wengine. Mtiririko huu hufanya uwepo wa nguvu, virutubisho, na hewa ya kaboni, ambavyo kwa pamoja hutengeneza rutuba kwenye udongo.


Utunzaji wa rutuba ya udongo unaongozwa na filosofia hii ‘Lisha udongo ili nao ulishe mimea.’ Udongo wenye rutuba utazalisha mimea yenye afya inayoweza kukabiliana na magonjwa. Uzalishaji wa mazao kwa njia za asili uhakikisha kunakuwepo uzalishaji wa kutosha bila ya kutumia pembejeo za ziada isipokuwa matandazo, mboji na bila kutifua udongo mara kwa mara. Ongezeko la malighafi za asili husaidia kuimarisha udongo na kufanya kuwepo kwa virutubisho vya kutosha.


Athari kwa afya ya mimea


Kwa bahati mbaya, aina ya kilimo cha kisasa na kinachotumia kemikali hufanywa tofauti na ilivyo kwa kilimo hai. Katika aina hii ya kilimo; udongo hulimwa mara kwa mara jambo linalosababisha uharibifu wa muundo wa udongo, uwiano wa virutubisho, ambapo virutubisho huongezwa kwa kutumia mbolea za viwandani na matandazo hayazingatiwi. Muundo wa udongo unapobadilika, rutuba nayo hupungua, uwezo wa udongo kwenye udongo pia hupungua.


Kiwango cha udongo mzuri pia hupungua kwa kuwa hakuna tena viumbe hai wanaotengeneza udongo ila unapungua kila msimu wa mavuno. Kwa asili mzunguko huu huwa na matokeo yanayoishia kwenye afya ya mimea, na hapa wadudu huchukua nafasi inayowawezesha kufikia malengo yao.


Ziba pengo


Wakulima wanatakiwa kuhakikisha kuwa kuna virutubisho vya kutosha shambani mwao kila wakati. Ikiwa kuna mwanya pale ambapo baadhi ya pembejeo zinakosekana, kununua virutubisho kwa ajili ya udongo vilivyomo kwenye mfumo wa mbolea za asili inaruhusiwa. Hata hivyo, weka utaratibu wa kuwa na virutubisho kutoka shambani mwako muda wote.


Endapo tukitegemea kulisha udongo kutokana na mbolea za viwandani na kutumia virutubisho vya asili, bado tutakuwa tunafanya sawa na yanayofanyika katika kilimo cha kisasa. Tutakuwa hatujauongezea udongo uwezo wa kujitengeneza na kuongezeka, jambo ambalo ndio msingi muhimu wa kilimo hai.


Vyanzo vya virutubisho


Mimea inayofunika udongo – Mimea inayotambaa huongeza na kushika virutubisho kwenye udongo, kuongeza malighafi zinazooza kwenye udongo, kuzuia madini ya naitraiti kuzama kwenye udongo, virutubisho kutiririshwa, na mmomonyoko wa udongo. Jambo la muhimu hapa ni kuwa udongo umefunikwa ili kuzuia uharibifu. Mimea jamii ya mikunde inapendekezwa zaidi kwa kuwa
husaidia kuongeza nitrojeni kwenye udongo inayopatikana hewani.


Inashauriwa pia kuchanganya mimea jamii ya mikunde na nyasi kwa kuwa nyasi hutumia nitrojeni nyingi sana kutoka kwenye udongo, hivyo itasaidia kutokuharibika kwa mtiririko mzima wa uwekaji wa nitrojeni kwenye udongo.


Mboji - Mboji hasa inayotengenezwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama, inaweza kuwa chanzo kizuri cha viumbe wadogo kwenye udongo na virutubisho vyenye gharama ndogo. Unapotumia mboji, changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa imeoza vizuri na namna ya kuitumia kwa usahihi. Endapo mchanganyiko uliotumika kutengeneza mboji hiyo yalikuwa na ubora wa chini, basi mboji hiyo nayo itakuwa na ubora mdogo sana. Itakuwa vizuri kama wakulima hawataacha mboji ikapigwa na jua au mvua, kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha kupotea kwa virutubisho kwenye mboji. Kinyesi cha mifugo huboresha mboji zaidi.


Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa kiasi cha 15% ya virutubisho vinavyopatikana kwenye mboji hutumika shambani kwa mwaka wa kwanza. Hivyo, matumizi ya mara kwa mara ya mboji yanapendekezwa ili kuweza kuongeza nitrojeni na malighafi zinazo oza kwenye udongo.


Samadi - Samadi inayotokana na wanyama waliokomaa inaweza kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho vya nitrojeni na aina nyingine kwa kiasi kidogo. Tatizo moja la samadi ni upatikanaji pamoja na kutokuwa na ubora unaofanana wakati wote. Kiasi kikubwa cha samadi inayotumika kwenye shamba la mboga, huozeshwa kabla ya kutumika, jambo linalosaidia kupunguza madhara kwenye vyakula.


Malengo kwa ajili ya udongo na mazao
•  Kuongeza malighafi zinazo oza kwenye udongo
• Kuboresha muundo wa udongo
• Kuwezesha upatikanaji wa nitrojeni
• Kuongeza uwezo wa uhifadhi wa rutuba
• Kujenga uwepo wa uhai wa viumbe hai kwenye udongo
• Kufifisha magonjwa ya mazao
• Kujenga mazingira ya udongo wenye uwiano

Chanzo: Mkulima Mbunifu