Thursday, July 7, 2011

KILIMO NA MAENDELEO YA TANZANIA



Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Kilimo kinachukua takribani nusu ya pato zima la taifa na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nchi za nje. Pamoja na kutoa chakula, kilimo vile vile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania. Sehemu kubwa ya kilimo Tanzania ni cha wakulima wadogo-wadogo (small-holder farmers, au peasants) ambao mashamba yao yana ukubwa wa kati ya hekta 0.9 na hekta 3.0 kila moja. Karibu asilimia 70 ya ardhi ya ukulima wa mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 kwa kutumia maksai na asilimia 10 kwa kutumia trekta. Kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua. Uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaoongoza katika uchumi wa Kilimo. Hekta milioni 5.1 zinalimwa nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula tu. Wanawake ndiyo wafanyakazi wakubwa mashambani. Matatizo makubwa yanayokabili Kilimo nchini Tanzania ni upungufu wa nguvu kazi na uzalishaji kutokana na uhaba wa nyenzo za kisasa za ukulima pamoja na kutegemea sana hali ya hewa ambayo haiaminiki. Mazao na wanyama huathirika vibaya sana nyakati za ukame. Kilimo cha umwagiliaji maji ndicho ambacho kinaweza kuinusuru Tanzania katika kuhakikisha uzalishaji usioterereka ili kujenga akiba nzuri ya chakula, pamoja na kuongeza kipato na kuboresha uzalishaji wa mazao kwa mkulima.
Uzalishaji Katika Kilimo
Pato la ndani ya nchi la Kilimo limekuwa kwa kiwango cha asilimia 3.3 kwa mwaka kuanzia mwaka 1985. Mazao ya chakula yaliongezeka kwa asilimia 3.5, na mazao ya biashara kwa asilimia 5.4 kwa mwaka. Serikali ya tanzania inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Vilevile inatilia maanani vichocheo vyote vinavyotoa msukumo wa uzalishaji katika kilimo kama vile miundombinu, huduma za fedha vijijini, umilikaji ardhi na utawala bora. Ili kufanikisha azma hiyo, hatua mbalimbali sasa hivi zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika kilimo kwa wakulima wadogowadogo na wale wakubwa wa kibiashara. Serikali vilevile inajitahidi kuongeza mgao wake wa bajeti kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya kilimo kwa ujumla.

Mazao ya Chakula
Tanzania imejaliwa kuwa na aina nyingi za kilimo kutegemeana na hali ya hewa na mazingira ya nchi. Mazao makubwa ya chakula ni: mahindi, mtama, mpunga, ngano, maharage, muhogo, viazi na ndizi.
Mazao ya Biashara
Kahawa, pamba, korosho, tumbaku, katani, alizeti, majani ya chai, karafuu, mazao ya bustani, ufuta, viungo vya chakula na maua.
Maeneo ya Kilimo
Nyanda za pwani, mabonde na safu za milima ya mashariki, nyanda za juu za kusini, Bonde la ufa la Kaskazini, milima ya volkeno, Bonde la Kati, Rukwa – Bonde la Mto Ruaha, sehemu za matope za bara, ufipa na Nyanda za Juu za Magharibi.
Kilimo cha Kumwagilia Maji
Tanzania inao uwezo wa kuendeleza kilimo cha kumwagilia ili kuwa na uhakika wa akiba ya chakula ya kudumu pamoja na kuboresha viwango vya maisha ya watu wake. Maji yanapatikana kwa wingi katika mito mikubwa na midogo pamoja na maziwa na mabwawa. Eneo ambalo linaweza kuwekwa chini ya kilimo cha kumwagilia maji ni hekta milioni 1.0, lakini mpaka hivi sasa ni hekta 150,000 tu zinazolimwa kwa kumwagilia maji.
Uwekezaji katika Kilimo
Mashirika yafuatayo, ambayo yako chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula, ni vitega uchumi vizuri vya uwekezaji kwa wale wanaotaka kuyanunua, au kuingia ubia na Serikali.

• Shamba la Kahawa la Mbozi lenye eneo la hekta 409.32. Mashamba haya yako Ishera, Ndungu, Tukumbi, Ng’amba, Ihanda na Hauseketwe.
• Kampuni ya Korosho na viwanda vyake vilivyoko Mtwara, Kibaha, Likombe, Masasi, Newala, Tanita dar es Salaam, Lindi, Nachingwea na Tunduru.
• Kampuni ya Usagishaji ya Taifa na vinu vyake vilivyoko Isaka, Tabora, Shinyanga, Mtwara na Iringa (vyote vya mpunga); na vinu vingine vya mahindi na mtama vikiwa Mwanza, Mtwara na Arusha. Mali za kampuni ni pamoja na majengo ya kuishi.
• Kampuni ya Mashamba Bagamoyo (Bagamoyo Farms Ltd.).
• Kampuni ya Mbegu ya taifa (Shamba la Kwamtili).
• Mashamba ya Mpunga ya Dakawa na Mbarali, mashamba ya mahindi ya Ruvu na miradi ya Kapunga, Madibira, Mbozi na Namtumbo.
• Mashamba ya Ngano na Karakana Basutu, Gawal, Gidagamwd, Mulbadaw, Murandja, Kampuni ya Ngano ya Seteet, Warret na Kituo cha kati cha matengenezo ya Ufundi (CMSC).
• Mashamba ya sukari yanayomilikiwa na Chuo cha Sukari cha Taifa na Kampuni ya Sukari ya Kagera.
• Viwanda vya mazao ya Kilimo.

Chanzo: www.tanzania.go.tz/kilimo.html

No comments:

Post a Comment