Pages
▼
Saturday, February 18, 2012
JK: Sekta binafsi ziwekeze katika kilimo
RAIS Jakaya Kikwete, amesema sekta YA kilimo inaweza kukua kwa kiasi kikubwa kama tu sekta binafsi za ndani na nje ya nchini, zitajikita katika uwekezaji ndani ya sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa mageuzi ya kilimo uliowakutanisha mawaziri wa kilimo kutoka nchi saba barani Afrika, mabalozi, wawekezaji na mashirika mbalimbali jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema ili nchi za Afrika zipige hatua katika kilimo, lazima ziwashirikishe wawezekaji wa sekta binafsi.
“Tunapaswa kuishirikisha sekta binafsi katika kuinua kilimo na kujenga viwanda vya kuzalishia mbegu bora,” alisema Rais.
Alisema mkutano uliofanyika Dar es Salaam kuhusu kilimo, uliangalia zaidi uwekezaji katika mikoa inayojitosheleza kwa uzalishaji wa chakula, ambayo ni Mbeya, Rukwa, Iringa, Ruvuma, Morogoro na Kigoma
Alisema mkutano huo uliazimia kuwatafuta wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi, ili watafute njia bora ya kuwasaidia wakulima wadogo.
“Hawa wawekezaji tulikubaliana kuwa wakija kufanya shughuli zao za kilimo, wawashirikishe pia wakulima wadogo,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika mpango huo unaozihusisha nchi za Tanzania, Rwanda, Ghana, Burkina Faso, Msumbiji na Kenya, utakuwa mfano mzuri kwa nchi nyingine za Afrika.
“Hapa Tanzania tuna mpango mzuri wa Kilimo Kwanza, mpango ambao kwa kweli umezivutia nchi nyingi Afrika,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe, alisema usalama wa chakula hauwezi kuimarika kama hakutakuwa na njia bora za kuinua sekta ya kilimo.
Alisema wakati umefika wa kuondokana na mfumo wa familia moja kuzalisha magunia nane ya mazao mbalimbali na badale yake kuwa na mfumo wa kuzalisha magunia 400 kwa kutumia njia za kilimo za kisasa na si kwa kutumia jembe la mkono
Profesa Maghembe alisema moja ya masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni kuboresha kilimo, kwa kuhimiza matumizi ya mbegu bora, mbolea na dawa ya kuzuia mazao kushambuliwa na wadudu.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Kenya, Dk Sally Kosgei, aliliambia Mwananchi kuwa tatizo kubwa linalozifanya nchi za Afrika kukumbwa na njaa mara kwa mara ni mabadiliko ya hali ya hewa.
Dk Kosgei alisema ili kuondokana na hali hiyo, nchi za Afrika zinapaswa kitu kimoja na kushirikiana katika kuleta mapinduzi kwenye kilimo.
Mkutano huo utakaokuja na mapendekezo ya pamoja kuhusu jinsi ya kuinua sekta ya kilimo katika nchi za Afrika, ulianza juzi na kumalizika jana.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment