Pages

Thursday, September 23, 2010

UMUHIMU NA NAFASI YA VIKUNDI KATIKA MAENDELEO

Vikundi vya maendeleo, ni jukumuiko la wananchi wakeleketwa wenye nia ya kuleta mabadiliko kwa kutumia uwezo na ubunifu wao katika kuamasisha ari ya wananchi kushiriki kwa pamoja katika kutafakari na kutafuta ufumbuzi wa jambo linalohitaji kutafutiwa suluhu. Vikundi vya maendeleo kama ya Elimu, Uchumi, ushawishi na utetezi, kilimo, ufugaji, ujasiriamali, uchangishaji wa fedha, na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Katika shughuli hizo vikundi vinaweza kuwa kiungo muhimu na imara katika kusonga mbele kwa maendeleo ya wanakikundi wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla wake kwa kutumia vikundi katika maeneo yetu; tunaongeza ubunifu, ufumbuzi wa mambo mbalimbali na kuongeza msukumo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Uhuru wa kushirikiana katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ibara ya 18 na 20 za katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzannia zimeweka wazi juu ya haki na uhuru wa mtu binafsi na kikundi kutoa mawazo, maoni au kushirikiana na wengine ili kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Yafuatayo yameainishwa wazi kwenye katiba kuhusu haki na wajibu wa jamii na uwepo wa vikundi kwa ajili ya maendeleo:-
Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni na kueleza fikra zake.
Kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi.
Kila mtu anao uhuru wa kufanya mawasiliano yake na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.
Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Kila mtu anao uhuru wa kukutana na kushirikiana na wengine kwa ajili ya kutoa mawazo yake hadharani na kuanzia na kujiunga na vikundi, vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi, kuendeleza maslahi yake au maslahi mengineyo.
Nguvu na wajibu wa wananchi kuleta mabadiliko kupitia vikundi kwa dhana ya kufanya kazi ya pamoja
Mtu mmoja anapofanya kazi peke yake ni vigumu kubadilisha hali fulani. Anaweza akakosa ujasiri wa kuleta mabadiliko, kuchukua hatua au kutoa maoni na kero zake. Badala yake kikundi cha watu wenye nia madhubuti na imani sawa kuhusu hali fulani wanaweza wakafanya mambo makubwa. Kwa kufanya kazi pamoja na kusaidiana; mabadiliko yanaweza kupatikana tena kwa haraka zaidi. Kufanya kazi pamoja kunasaidia pia kujenga tabia ya kujiamini kama mawakala wa mabadiliko (egents for change ). umoja pia unarahisisha kupata msaada kutoka nje au ndani ya jamii kuliko msaada huo kutolewa kwa mtu au mwanaharakati mmoja.
Kwa ufupi vikundi vina faida zifuatazo:-
Kujenga nguvu na utashi wa pamoja (umoja ni nguvu)
kurahisisha utendaji wa pamoja.
Kubadilishana uzoefu (Kutiana moyo).
Kuelimishana.
Kushirikiana katika matumizi ya rasilimali.
MAKUBALIANO YA KUJIUNGA, KUANZISHA NA KUENDELEZA KIKUNDI
Kuwepo kwa nia ya pamoja.
Kabla ya kuunda kikundi ni lazima kuwepo tatizo/matatizo yanayowaunganisha wanachama wa kikundi na kukubaliana kushirikiana kuyakabili. Wanakikundi wanatakiwa kutambua umuhimu wa kuunganisha nguvu zao kutatua tatizo/matatizo hayo. Pakiwa na haja na nia ni rahisi kwa wanakikundi kukubaliana kwa pamoja kwa kuwa kila mmoja analiona tatizo lililo mbele yake.

Uhiari na utayari wa kujiunga na kikundi
Kimsingi, kujiunga na kikundi ni suala la hiari na kuwa tayari kujitolea kufanya kazi kwa pamoja ili kujiletea maendeleo yao. Kabla ya kujiunga au kuanzisha kikundi ni lazima kila mwanakikundi awe ameamua kwa hiari yake bila kushurutisha au, kushirikizwa maa mtu/taasisi yoyote. Endapo uamuzi wa kuanzisha/kujiunga katika kikundi utakuwa wa kulazimishwa haitakuwa rahisi kwa wanakikundi kukabili majukumu au wajibu kama mwanakikundi.

Tathmini ya aina na msingi wa kikundi
Kikundi kinaweza kuwa chombo kinachojitegemea au kikawa ni sehemu ya kikundi kimoja au taasisi fulani. Uanzishwaji na uendelezwaji wake unategemea sana wanachama wake, hivyo ili kuwa na kikundi chenye sauti na nia moja kuna haja kwa wanachama wake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kikundi kwa hiari na kwa kujituma. Siyo vizuri kwa kikundi kuwa tegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji na usimamizi wa shughuli zake.
Msaada toka kwa wadau wengine nje ya kikundi usiwe kipambele bali kichocheo tu katika kuleta mabadiliko. Ili kuleta mwelekeo mzuri wa vikundi hivi, huna haja ya wanakikundi kufanya tathmini yakinifu kutambua aina ya wanachama walionao. Kama kikundi kitakuwa na wanachama wenye moyo wa kujitolea na walio tayari kuleta maendeleo ya kweli basi kikundi hakitaishi kwa utegemezi wa msaada kutoka nje hususani kwa wahisani.

Wanachama mchanganyiko na ushiriki wa makundi maalumu.
Kuwa na kikundi chenye wanachama mchanganyiko wajinsia na makundi mbalimbali ya watu kunatoa fursa ya kujenga kikundi imara chenye uwakilishi sawia. Vikundi vya maendeleo havina budi kuwa na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya watu walioko ndani ya jamii kama vile watu wenye ulemavu, wanawake na wajane, maana makundi haya yanahitaji msaada na uprndeleo maalumu katika kushirikishwa katika maamuzi na pia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kujenga mahusiano mazuri
ni vyema kuwa na mahusiano ya karibu (kiutendaji) na watendaji mbalimbali katika ngazi ya kijiji, kata na wilaya. Ni vyema pia kwa kikundi kuzifahamu sera mbalimbali, sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya vikundi.
Kujali maslahi ya jamii na nchi
Kikundi kinatakiwa kuwa na mikakati inayochangia na kuchochea maendeleo endelevu ndani ya jamii na nchi kwa ujumla kwa kulingana na sera zilizokubaliwa na wanachama na nchi hali hiyo, kuna umuhimu wa wanachama kuchangia ili kuleta maslahi ya jamii pamoja kulingana na makubaliano ya wanakikundi na wananchi kwa ujumla.

Haja ya kupima utendaji wa kikundi
Kwa kuwa lengo kuu la vikundi ni kutetea na kuchochea maendeleo ya nchini, ni vizuri kikundi kikajenga tabia ya kupima utendaji wake ili kuona ni kwa kiasi gani wamefanikiwa au kutofanikiwa katika kuyafikia malengo na ndoto zao. Kikundi kinapaswa kujua hatima ya jitihada zake ili kuwa na hakika na kile kinachofanywa. Pia kikundi kinaweza kuonisha viashiria walivyojiwekea na vile vilivyowekwa na mipango/mikakati ya serikari na jumuia ya kimataifa.
Vikundi ni mojawapo ya mihimili itakayokuwa na nguvu kuleta maendeleo katika jamii husika. Vikundi havina budi kujipanga vyema ili kuweza kuhimili mikiki mikiki ya harakati za maendeleo ya jamii.
Pia, vikundi havina budi kufuata taratibu na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuepuka kuwa na mitazamo ya kidini, ushabiki wa kisiasa, Ukabila, ubaguzi wa aina yoyote ile na vitendo vya kihuni.

No comments:

Post a Comment