Mazao yaliyostawi vizuri yakionyesha mojawapo ya aina ya kilimo Asili cha Mseto
Wadau wa kilimo, sera, mazingira, utawala, na mashirika ya
kimataifa, wametoa wito wa kubaini mifumo asili ya Kilimo kwa kutambua
mchango katika uhakika wa chakula na kipato.Wito huo ulitolewa katika warsha iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyojumuisha wadau hao ili kutathmini mchango wa mifumo asili ya kilimo na changamoto zilizopo ili kuiboresha na kiendeleza.
Ilibainika kuwa Tanzania ina mifumo mingi ya asili ya kilimo na mifugo ambayo imedumu kwa taribani zaidi ya miaka 100 hadi 700.
Katika kipindi hicho, mifumo mingi imekumbana na mabadiliko ya hali ya hewa lakini imekabili na kudumu, hii inaonyesha kuwa kuna vitu vingi vya kujifunza katika mifumo hiyo.
Aidha, wadau wamependekeza mifumo ya asili ya kilimo na ufugaji kuingizwa katika sera kati ya zilizopo ili ipate nguvu ya kusimamiwa na kuendelezwa hasa ikizingatiwa umuhimu wake katika kuimarisha usalama wa chakula na kipato kwa kaya na taifa kwa ujumla.
Pia wametaka mashirika ya kimataifa yaendelee kuchangia kwa rasilimali uendelezaji wa mifumo asili endelevu kwani manufaa yake ya mazingira ni ya ulimwengu.
Afisa Mkuu wa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Firmat Banzi alisema kuwa mifumo asili ya kilimo ina haja ya kuendelezwa ili kuboresha na kuimarisha maarifa asili kuwezesha ushiriki wa wakulima katika utunzaji wa mifumo hiyo.
Alifafanua kuwa uendelezaji wa mifumo hiyo utawapa fursa wakulima kuweza kushiriki kikamilifu katika kilimo wakiwa na uhakika wa kupata mazao mengi kuweza kujitosheleza kwa chakula na kujiongezea kipato pamoja na kuboresha hifadhi ya mazingira hasa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Washiriki kwa pamoja wamepitisha azimio linalotambua mchango wa mifumo ya asili ya kilimo na ufugaji na wametoa wito wa kubaini mifumo asili iliyopo nchini, kutathmini mchango wake na changamoto kwa lengo la kuiboresha na kuiendeleza.
No comments:
Post a Comment