JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAWIZARA YA KILIMO
CHAKULA NA USHIRIKA
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI ZA VYAKULA MIKOANI
UTANGULIZI:
Tulianza msimu huu 2012/13 tukiwa na ziada kidogo ya
chakula na kwa kujitosheleza kwa asilimia 113. Msimu huu, tofauti na msimu
uliopita hatukuzuia wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi.
Pamoja na uzalishaji tuliokuwa nao katika maeneo kadhaa
ya nchi kulikuwepo na maeneo ambayo uzalishaji wake haukuwa wa kuridhisha
kutokana na hali mbaya ya hewa na hivyo kuwa na upungufu wa chakula. Upungufu huu unajidhihirisha kutokana na
kupungua kwa uingiaji na upatikanaji wa
vyakula sokoni, hususani unga wa mahindi ambacho ni chakula kikuu na bei ya soko kupanda sana kwa viwango vilivyo juu ya bei ya wastani
nchini.
Uchambuzi wa bei za vyakula unaonesha kwamba bei ya
wastani ya mahindi kitaifa ni shilingi 675 kwa kilo. Aidha, bei ya mahindi katika masoko ya miji
mkuu ya baadhi ya mikoa iko juu ya wastani.
Kwa mfano, bei ya Dar es Salaam tarehe 28 Novemba, 2012 ilifikia shilingi 750 kwa kilo, Mwanza shilingi 825, Moshi shilingi 700, Tanga shilingi 785, Tabora shilingi 750 na Mtwara shilingi 735. Aidha, unga wa sembe uliuzwa kati ya shilingi 1,100 na shilingi 1,500 kwa kilo, mwezi Desemba 2012.
Hali ilivyo katika maeneo mengi ya nchi ni kwamba, viwango
vya upatikanaji wa chakula vinatofautiana katika maeneo mbali mbali. Wakati mikoa minane (8) ya Iringa, Rukwa,
Mbeya, Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro ilikuwa na ziada ya chakula,
mikoa saba (7) ya Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida na Dodoma ilikuwa
na hali ya utoshelevu tu na mikoa sita (6) ya Shinyanga, Tabora, Arusha,
Kilimanjaro, Manyara na Dar es Salaam ilikuwa na uhaba wa chakula.
Kutokana na upungufu wa chakula kuzidi kujitokeza, mwezi
Oktoba, 2012, Serikali, kupitia Kamati ya Maafa iliidhinisha mgao wa tani
18,417.8 wa chakula cha njaa kutoka katika maghala ya Hifadhi ya Chakula ya
Taifa (National Food Reserve Agency) kwenda katika Halmashauri 35 za
mikoa 12 zilizobainika kuwa na upungufu mkubwa wa chakula. Mikoa iliyopewa chakula cha njaa ni Arusha,
Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga,
Singida, Tabora na Tanga.
Kutokana na hali ya
upungufu wa chakula kuzidi kuendelea na kujitokeza kwa majanga mengine kama
mafuriko, Serikali iliidhinisha mgao wa nyongeza ya chakula hadi kufikia tani
26,958.300 kwa Halmashauri zilizokuwa na
mahitaji makubwa ya chakula cha msaada. Aidha,
upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo yanayozalisha nafaka kwa wingi
umesababisha kupungua kwa chakula kinachosambazwa katika soko hivyo kufanya
usambazaji wa chakula kutolingana na mahitaji ya soko. Hali hii imesababisha
kupanda kwa bei ya mahindi na unga wa
mahindi katika baadhi ya masoko hususan ya mijini. Ili kukabiliana na hali hiyo Serikali
imechukua hatua zifuatazo:-
(i) Kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yaliyokuwa na
upungufu wa chakula.
Kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye upungufu wa chakula Serikali iliendelea
kuongeza mgao wa chakula cha msaada kutoka tani 18,417.8 hadi kufikia tani 28,250.300. Hadi kufikia mwezi Januari,
2013 jumla ya tani 19,040.865 za mahindi zilishachukuliwa. Aidha, jumla ya tani
9,209.435 bado hazijachukuliwa na mikoa iliiyopewa mgao wa nyongeza. Mikoa ambayo
bado haijachukua nyongeza hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Mbeya na Mara. Kiambatisho Na. 1
(ii) Kuuza tani 40,000 za mahindi kutoka kwenye ghala la Taifa
kwa ajili ya kushusha bei ya unga wa mahindi.
Serikali imeidhinisha kuuzwa tani 40,000 za mahindi
kutoka katika ghala la chakula la taifa ambapo tani 20,000 zitauzwa kati ya
mwezi Januari na Februari, 2013. Kwa bei ya shilingi 450 tu kwa kilo. Kiasi kingine
cha tani 20,000 kilichobaki kitauzwa kuanzia mwezi Machi katika maeneo
yatakayobainika kuwa na upungufu wa chakula na bei kuendelea kupanda. Mgao
Kimkoa ni kama inavyoonyesha kwenye Kiambatisho Na. 2.
2.
UTARATIBU WA KUUZA MAHINDI KWA WASAGISHAJI
Mikoa yenye bei ya
mahindi iliyo juu ya bei ya wastani kitaifa ndiyo iliyopewa mgao. Mikoa hiyo na mgao wake katika mabano ni kama ifuatavyo: Arusha (tani 1100), Dodoma (tani 400),
Kilimanjaro (tani 400), Lindi (tani 400), Mara (tani 900) , Manyara (tani 800),
Morogoro (tani 400), Mwanza (tani 2500), Shinyanga (tani 1029), Singida (tani
500), Tabora (tani 1000), Tanga (tani 700), Mtwara (tani 600) , Pwani (tani
700), Simiyu (tani 1971) na Dar es Salaam (tani 6400).
Utaratibu unaotumika kuuza mahindi kwa wasagishaji ni
kama ifuatavyo:
i.
Mikoa
imeelekezwa kuteua wasagishaji waaminifu wenye nia na uwezo wa kusagisha unga
kwa ajili ya kuuza kwa walaji kwa bei elekezi iliyopangwa na mkoa ambayo ni
kati ya shilingi 750 hadi 900 kwa kuzingatia gharama za usafirishaji.
ii.
Wasagishaji
walioteuliwa wanatakiwa kukidhi vigezo vilivyowekwa kama vile, uwezo wa kulipa
fedha za mahindi ndani ya muda uliopangwa, uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mahindi
anachonunua, uwezo wa kusagisha, kufungasha na kusambaza unga ndani ya siku
saba kuanzia siku aliyochukua mahindi, pamoja na kukubali kuuza kwa bei
elekezi.
iii.
Wasagishaji
walioteuliwa na mikoa watapewa vibali na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
ili waweze kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala kama
watakavyopangiwa.
iv.
Mikoa
itaingia mikataba na wasagishaji walioteuliwa na kusimamia utekelezaji wa
mikataba hiyo ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta
manufaa yaliyokusudiwa.
v.
Mikoa
itachukua hatua kwa msagishaji ambaye atabainika kutumia vibaya kibali
alichopewa, kama vile kuuza kibali hicho kwa msagishaji mwingine, kusafirisha
na kuuza mahindi au unga kwenye maeneo tofauti na aliyopangiwa, kutosagisha na
kuuza unga ndani ya siku saba kwa mujibu wa mkataba.
3.
UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUPUNGUZA BEI YA UNGA KWA WALAJI
Mikoa iliyopewa mgao imeelekezwa
utaratibu wa kununua mahindi kutoka katika maghala ya Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula. Hadi kufikia tarehe 14 Januari, 2013 jumla ya mikoa 11 kati ya Mikoa 16 ilikuwa
imewaslisha orodha ya wasagishaji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Mikoa
hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Morogoro, Lindi, Mtwara,
Pwani,Tanga na Dar es Salaam. Mikoa ambayo haijawasilisha orodha ya
wasagishaji ni Mwanza, Tabora, Shinyanga, Mara.
Kuendelea kuchelewa kuwasilisha orodha ya wasagishaji
kunasababisha kuchelewesha zoezi zima la utoaji wa mahindi, usafirishaji,
usagishaji na hivyo kuchelewesha unga kuingia sokoni hali inayosababisha bei
kuendelea kupanda. Mikoa hiyo inaagizwa
kuwasilisha orodha ya wasagishaji ndani ya siku
saba kuanzia sasa. Jumla ya
wasagishaji 127 tayari wameshapewa
vibali vya kununua mahindi yanayofikia tani 12,520.00 ambapo tani 7,858.291
zimeshalipiwa na uchukuaji unaendelea lakini kasi ya kulipia na kuchukua ni
ndogo. Orodha ya Wasagishaji kama ilivyowasilishwa na mikoa na kiasi walichoidhinishiwa
kununua imeoneshwa katika Kiambatisho Na.3.
Serikali inawaagiza Wasagishaji wote waliopewa vibali vya
kununulia mahindi kuhakikisha wanalipia na kuchukua kiasi chote cha mahindi
kama walivyoidhinishiwa katika vibali vyao ndani ya siku saba kuanzia sasa, vinginevyo Serikali italazimika kufuta
vibali hivyo na kuvigawa upya kwa Wasagishaji wengine katika mikoa husika wenye
nia thabiti ya kufikisha unga sokoni.
4. USIMAMIZI NA
UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaagizwa kusimamia na kufuatilia
kikamilifu utekelezaji wa zoezi hili kama ilivyoelekezwa. Aidha, mikoa
inatakiwa kuweka mfumo mzuri wa usimamizi na usambazaji wa unga unaotokana na
mahindi yaliyonunuliwa kutoka katika ghala la Serikali ikiwa ni pamoja na
kuwafahamisha wananchi maeneo ambayo unga huo unapatikana pamoja na bei elekezi
iliyopangwa na mikoa.
Katika ngazi ya Taifa
Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa utaratibu wa kufuatilia
utekelezaji wa mkakati huu katika mikoa yote iliyopata mgao wa chakula cha njaa
au mgao ulitolewa kwa wasagishaji kwa ajili ya kupunguza bei ya unga katika
masoko ya mijini.
5. MWISHO
Kwa kuwa maghala ya
Dar es Salaam (Kipawa), Arusha, Dodoma na Shinyanga yana upungufu wa akiba ya
chakula kulinganisha na mahitaji ya sasa katika maeneo hayo, Serikali inaendelea kuhamisha chakula kutoka
katika maghala yenye akiba ya kutosha kwenda katika maghala yenye upungufu ili kurahisisha
usambazaji wa chakula katika maeneo yenye upungufu. Tunaendesha zoezi hili la
kuhamisha chakula kwa kutumia Shirika la
Reli (TRL) , Jeshi la Wananchi na wasafirishaji binafsi ili kuhakikisha kwamba
chakula kinafika haraka.