Pages

Monday, April 16, 2012

Matumizi ya ardhi yashirikishe jamii

MIGOGORO ya ardhi imeendelea kuzikumba jamii nyingi katika maeneo mbalimbali nchini hivyo kusababisha migogoro.
Jamii inatumia muda mwingi kutatua migogoro hiyo badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, ardhi ndio tegemeo kubwa kwa jamii za wakulima na wafugaji ambao ndio sehemu kubwa ya Watanzania.

Ardhi ndio mtaji pekee ambao Watanzania wengi waishio vijijini wanaitegemea kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuweza kuwapatia chakula na kipato.

Licha ya kuwepo kwa mamlaka zinazohusika na usimamizi pamoja na ugawaji wa ardhi, migogoro hiyo imeendelea kuwa sehemu ya maisha kwa jamii nyingi.

Kama sheria za usimamizi na umiliki wa ardhi zipo, kitu gani kinasababisha migogoro ambayo inagharimu maisha na mali za Watanzania wasio na hatia?

Sisi tunasema kuwa, sheria za ardhi zinatoa haki ya kutumia ardhi na si kuimiliki hivyo inatosha kumhakikishia mtu kuwa, kitu chochote ambacho atakiendeleza katika ardhi husika, kitalindwa kwa maslahi yake si lazima kumwambia ardhi hiyo ni yako ili aiendeleze.


Migogoro ya ardhi husababishwa na mambo mbalimbali ambayo baadhi yake ni upungufu katika sheria za ardhi, mamlaka zinazohusika na ugawaji wa viwanja kugawa kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja na fidia ndogo.

Licha ya kufanyika marekebisho katika sheria za kusimamia matumizi ya ardhi, bado migogoro hiyo imeendelea kuchukua nafasi miongoni mwa jamii nyingi za Kitanzania.

Upo umuhimu mkubwa wa kushirikisha jamii katika kufanya maamuzi yanayohusu matumizi ya ardhi. Kama wananchi watashirikishwa, migogoro mingi iliyopo vijiji itapungua.

Ipo tabia ya baadhi ya Halmashauri za vijiji, kupitisha taarifa feki inayoamua matumizi ya ardhi ya kijiji bila ridhaa ya wananchi.

Serikali nayo inachangia migogoro hii pale inaposhindwa kulipa fidia kwa wananchi baada ya kutwaa ardhi kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Umefika wakati wa wananchi kuelimishwa juu ya sheria mbalimbali za ardhi ili watambue haki na wajibu wao katika suala zima la umiliki na matumizi ya yake.

CHANZO; MAJIRA

No comments:

Post a Comment