Pages

Wednesday, February 29, 2012

PASS kusaidia maendeleo ya kilimo

Asasi ya Kusaidia Uwekezaji Kwenye Kilimo (PASS) imeanzisha huduma mpya zitakazo rahisisha upatikanaji wa mikopo inayolenga kusaidia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa PASS, Iddy Lujina, katika mkutano ulioshrikisha mabenki mbalimbali kwa ajili ya kuzitambulisha huduma hizo mpya kwa lengo la kusaidia kilimo.

“Tumeona kuna umuhimu wa kuongeza upatakanaji wa huduma zetu kwa wadau wengi zaidi kwa maendeleo ya sekta hii nyeti nchini,” alisema, Lujina.

Alisema huduma hizo mpya ni pamoja na kuwezesha mabenki kujiongoza zenyewe kufanya tathimni na kutoa mikopo kwa wakulima kwa dhamana ya mikopo iliyo chini ya Sh. milioni 15.

Kusaidia benki ndogondogo kupata mikopo kutoka katika mabenki makubwa ili nazo ziweze kutoa mikopo kwa wakulima wadogo.

Kusaidia kuanzisha mfuko wa dhamana wa asasi hiyo katika benki mbalimbali kwa ajili ya kukopesha wakulima bila kuhamisha dhamana hiyo kutoka benki moja kwenda nyingine.

Huduma nyingine ni kusaidia upatakanaji wa mashine na matrekta kwa ajili ya kukopesha wakulima kushiriki katika kilimo cha kisasa na kusindika mazao yao.

Lujina alisema hadi sasa wametoa matrekta 190, na wanahitaji kupanua zaidi huduma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kusaidia wakulima wengi zaidi.

Muwakilishi kutoka benki ya CRDB, Mussa Lwila, alisema benki hiyo inashirikiana na PASS kwa kipindi cha miaka kumi sasa na wameweza kuwafikia wakulima 300 nchi nzima wanaojishughulisha na kilimo kama mtu mmoja na makundi.

Mshauri wa PASS kutoka kampuni ya Inspired International, Richard Pelrine, alisema PASS imejipanga kuhakikisha wakulima wengi wanafaidika na mikopo toka taasisi hiyo kwa ajili ya kujiendeleza na nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment