Pages
▼
Monday, July 25, 2011
Wanarombo na changamoto ya uvamizi wa tembo mashambani
KUMEKUWEPO na malalamiko mengi katika jamii yanayohusu wanyama wa porini kuvamia makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mali na hata vifo.Malalamiko hayo yamekuwa yakilalamikia wanyamapori aina ya Tembo ambao mara kwa mara wamekuwa wakivamia makazi ya watu na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao,kuua wananchi,kujeruhi nahata kuwasababishia wengine ulemavu wa kudumu.
Moja ya maeneo ambayo wananchi wanalalamikia wanyama hao ni Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro ambapo wanyama hao wamekuwa wakivamia mara kwa mara na kusababisha uharibifu mkubwa.
Hisroria inaonesha kuwa Tembo wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali wilayani Rombo na kuvuka mpaka wa nchi ya Tanzania na Kenya katika majira mbalimbali kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.
Tembo hayo hupita katika Wilaya ya Rombo kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) Kimsingi Tembo hao wanashabihiana na tembo wanaopatikana katika Hifadhi
ya Taifa Tsavo na Ambusell zilizopo nchini Kenya
Akizungumzia tatizo la Tembo katika Wilaya ya Rombo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Peter Toima anasema kabla ya 1992 Tembo walikuwa wakipita mara mbili au Tatu katika miezi ya Mei,Juni na Julai katika kutafuta mahitaji yao mbalimbali wakitokea katika Hifadhi za Taifa za Tsavo Magharibi na Ambosell
za Kenya kupitia maeneo ya makazi na mashamba ya watu nakwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Anasema katika kipindi hicho uharibifu ulikuwa ni mdogo na hakukuwepo na madhara makubwa kwa binadamu na mali zao.Anasema kuanzia 1992 hadi sasa Tembo walianza kula mazao mashambani nyakati za usiku mfululizo katika vijiji vya Kiraeni, Msaranga, Maorosha, Kitowo na Marangu ambapo viko katika Tarafa ya Mashati wilayani humo na vinapakana na nchi jirani ya Kenya.
“Uvamizi huo uliendelea kuongezeka kuanzia mwezi Machi hadi Oktoba ya kila mwaka hadi mwaka 2009 hali ambayo iliendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi na kuzua uhasama wa wananchi na wanyama hao,” anasema Bw. Toima.
Anasema kuanzia kipindi cha mwaka 2010 uvamizi wa Tembo katika mashamba na makazi ya watu umekuwa kwa kipindi chote cha mwaka hali ambayo inatokana na ongezeko la ukame hivyo kuwalazimu tembo kula mazao yaliyopandwa mashambani.
Kutokana na hali hiyo kumekuwepo na mgogoro mkubwa baina ya binadamu na Tembo ambao unachangiwa na sababu mbalimbali.
Anasema Moja ya sababu zilizochangia kuendelea kukua kwa mgogoro baina ya binadamu na Tembo ni Ongezeko la idadi ya watu ambalo limesbabisha mahitaji makubwa ya ardhi kwa wananchi hivyo kusababisha matumizi ya ardhi ambayo hapo awali yalikuwa hayatumiki kwa shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi
ya watu.
Anasema chanzo kingine kilichochangia kuongeze kwa migogoro ya Tembo na binadamu ni kuzibwa kwa mapito ya wanyamapori ambapo mapito hayo yamezibwa na shughuli za kiuchumi za binamu.
“Shughuli za kiuchumi za binadamu zimesababisha maeneo yaliyokuwa mapito ya Tembo kwenda sehemu ambazo walikuwa wanapata mahitaji yao muhimu hivyo kusababisha madhara kuwa pindi wanapopita mapitio hayo na kukuta yamevamiwa na makazi ya watu,”anasema.
Sababu nyingine ni Hali duni ya kipato kwa wananchi ambayo imesababisha wananchi kujishughulisha na uvunaji wa maliasili usioendelevu na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, Mfano ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni,ufunguaji wa mashamba mapya na uchomaji misitu moto.
Shughuli hizo zimesababisha kupunmgua kwa malisho ya Tembo na kuchochea mgogoro baina ya Tembo na binadamu.
Aidha anasema mabadiliko ya Tabia ya nchi nayo yamesababisha Tembo kukosa malisho na kuvamia makazi ya watu kwa ajili ya kutafuta chakula na maji hivyo kusababisha kero kwenye mashamba na makazi ya wananchi.
Bw.Toima anasema maeneo yanayoathiriwa na Tembo katika wilaya hiyo ni Tarafa ya Mengwe vijiji vya Mamsera Chini, Holili, Mahida, Ngoyoni, Ngaren, Mengenichini na Aleni chini, Tarafa ya Mkuu vijiji vya Shimbi Mashariki na Ikuini pamoja na Tarafa ya Mashati vijiji vya Kiraeni, Msaranga,Maharosha,Kitowo na
Marangu.
Maeneo mengine ni Tarafa ya Useri vijiji vya Kirongo chini na leto pamoja Tarafa ya Tarakea katika msitu wa kustawishwa wa Rongai maeneo ya Kamwanga,Rongai,Endoneti,Nalemuru na vijiji vinavyopakana na msitu wa ukanda wa Nusu mail ambavyo ni Kikelelwa, Mbomai na Nanjara.
Akizungumzia tatizo la uharibifu wa wanyama pori mhifadi katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (KINAPA), Bw. Emanuel Moirana anasema kipindi ambacho wanyamapori hususani tembo wanahamia kukidhi mahitaji yao husababisha uharibifu mkubwa katika vijiji wanavyopita.
Bw.Moirana anasema uharibifu huo ni pamoja na kuharibu Mazao, kuua mifugo na mara nyingine kuleta madhara kwa binadamu na hata kifo.
Anasema uharibifu ambao hufanywa na wanyamapori ni kuvamia mashamba katika maeneo wanayopita na maeneo yaliyokandokando ya hifadhi pamoja na kuvamia mifugo katika malisho na hata katika maboma.
Uharibifu mwingine ni wa miundombinu ya maji kama
mabomba,kujeruhi,kisababisha vifo kwa binadamu hasa jamii za wafugaji wanaojaribu kulinda mifugo yao ama wakulima ambao mara nyingi hushambuliwa wakiwa mashambani.
Anasema sababubu inayochangia migogoro baina ya wanyama pori na binadamu ni mapitio ya wanyama kuvamiwa na kukaliwa na binadamu pamoja na ongezeko la idadi ya watu katika maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyama na uhamaji wa kawaida wa wanyama hao.
Aidha anaeleza kuwa wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuwadhibiti wanyama hao ikiwa ni pamoja na kuweka uzio wa waya wa umeme,uzio wa miti mifano ya Michongoma,kuchimba mitaro kuzunguka eneo husika pamoja na kutumia pilipili.Anasema njia nyingine ambayo wanatumia kuwadhibiti wanyama hao ni kufanya doria za kufukuza wanyama hao na kuwasumbua ambapo askari hufanya doria mara kwa mara aidha kwa miguu au kwa gari kuzungukia eneo lililo na wanyama na kuwafukuza kwa kuwatishia kwa risasi za moto na risasi baridi.
Aidha anasema ili kuweza kudhibiti wanyama hao serikali za vijiji zinapaswa kuwa na mpango bora wa matumizi ya Ardhi na kuutekeleza.Anasema mpango huo uainishe maeneo maalumu kwa ajili ya makazi ya raia,maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo,maeneo ya Kilimo pamoja na maeneo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi maliasili
“Utekelezaji wa mpango huu utasaidia kuepusha migogoro inayotokana na migogoro kati ya wanyama na binadamu”anasema Bw.Moirana.
Bw. Moirana anasema pamoja na jitihada mbalimbali walizonazo za kudhibiti wanyamapori wasivamie katika mkazi ya watu,wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo bajeti kuwa finyu ikilinhanishwa na shughuli za kupambana na wanyama hao waharibifu.
Chanzo;
Flora Temba,Majira (Julai,2011)
No comments:
Post a Comment