Pages
▼
Monday, July 25, 2011
Wanarombo na changamoto ya uvamizi wa tembo mashambani
KUMEKUWEPO na malalamiko mengi katika jamii yanayohusu wanyama wa porini kuvamia makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mali na hata vifo.Malalamiko hayo yamekuwa yakilalamikia wanyamapori aina ya Tembo ambao mara kwa mara wamekuwa wakivamia makazi ya watu na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao,kuua wananchi,kujeruhi nahata kuwasababishia wengine ulemavu wa kudumu.
Moja ya maeneo ambayo wananchi wanalalamikia wanyama hao ni Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro ambapo wanyama hao wamekuwa wakivamia mara kwa mara na kusababisha uharibifu mkubwa.
Hisroria inaonesha kuwa Tembo wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali wilayani Rombo na kuvuka mpaka wa nchi ya Tanzania na Kenya katika majira mbalimbali kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.
Tembo hayo hupita katika Wilaya ya Rombo kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) Kimsingi Tembo hao wanashabihiana na tembo wanaopatikana katika Hifadhi
ya Taifa Tsavo na Ambusell zilizopo nchini Kenya
Akizungumzia tatizo la Tembo katika Wilaya ya Rombo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Peter Toima anasema kabla ya 1992 Tembo walikuwa wakipita mara mbili au Tatu katika miezi ya Mei,Juni na Julai katika kutafuta mahitaji yao mbalimbali wakitokea katika Hifadhi za Taifa za Tsavo Magharibi na Ambosell
za Kenya kupitia maeneo ya makazi na mashamba ya watu nakwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Anasema katika kipindi hicho uharibifu ulikuwa ni mdogo na hakukuwepo na madhara makubwa kwa binadamu na mali zao.Anasema kuanzia 1992 hadi sasa Tembo walianza kula mazao mashambani nyakati za usiku mfululizo katika vijiji vya Kiraeni, Msaranga, Maorosha, Kitowo na Marangu ambapo viko katika Tarafa ya Mashati wilayani humo na vinapakana na nchi jirani ya Kenya.
“Uvamizi huo uliendelea kuongezeka kuanzia mwezi Machi hadi Oktoba ya kila mwaka hadi mwaka 2009 hali ambayo iliendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi na kuzua uhasama wa wananchi na wanyama hao,” anasema Bw. Toima.
Anasema kuanzia kipindi cha mwaka 2010 uvamizi wa Tembo katika mashamba na makazi ya watu umekuwa kwa kipindi chote cha mwaka hali ambayo inatokana na ongezeko la ukame hivyo kuwalazimu tembo kula mazao yaliyopandwa mashambani.
Kutokana na hali hiyo kumekuwepo na mgogoro mkubwa baina ya binadamu na Tembo ambao unachangiwa na sababu mbalimbali.
Anasema Moja ya sababu zilizochangia kuendelea kukua kwa mgogoro baina ya binadamu na Tembo ni Ongezeko la idadi ya watu ambalo limesbabisha mahitaji makubwa ya ardhi kwa wananchi hivyo kusababisha matumizi ya ardhi ambayo hapo awali yalikuwa hayatumiki kwa shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi
ya watu.
Anasema chanzo kingine kilichochangia kuongeze kwa migogoro ya Tembo na binadamu ni kuzibwa kwa mapito ya wanyamapori ambapo mapito hayo yamezibwa na shughuli za kiuchumi za binamu.
“Shughuli za kiuchumi za binadamu zimesababisha maeneo yaliyokuwa mapito ya Tembo kwenda sehemu ambazo walikuwa wanapata mahitaji yao muhimu hivyo kusababisha madhara kuwa pindi wanapopita mapitio hayo na kukuta yamevamiwa na makazi ya watu,”anasema.
Sababu nyingine ni Hali duni ya kipato kwa wananchi ambayo imesababisha wananchi kujishughulisha na uvunaji wa maliasili usioendelevu na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, Mfano ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni,ufunguaji wa mashamba mapya na uchomaji misitu moto.
Shughuli hizo zimesababisha kupunmgua kwa malisho ya Tembo na kuchochea mgogoro baina ya Tembo na binadamu.
Aidha anasema mabadiliko ya Tabia ya nchi nayo yamesababisha Tembo kukosa malisho na kuvamia makazi ya watu kwa ajili ya kutafuta chakula na maji hivyo kusababisha kero kwenye mashamba na makazi ya wananchi.
Bw.Toima anasema maeneo yanayoathiriwa na Tembo katika wilaya hiyo ni Tarafa ya Mengwe vijiji vya Mamsera Chini, Holili, Mahida, Ngoyoni, Ngaren, Mengenichini na Aleni chini, Tarafa ya Mkuu vijiji vya Shimbi Mashariki na Ikuini pamoja na Tarafa ya Mashati vijiji vya Kiraeni, Msaranga,Maharosha,Kitowo na
Marangu.
Maeneo mengine ni Tarafa ya Useri vijiji vya Kirongo chini na leto pamoja Tarafa ya Tarakea katika msitu wa kustawishwa wa Rongai maeneo ya Kamwanga,Rongai,Endoneti,Nalemuru na vijiji vinavyopakana na msitu wa ukanda wa Nusu mail ambavyo ni Kikelelwa, Mbomai na Nanjara.
Akizungumzia tatizo la uharibifu wa wanyama pori mhifadi katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (KINAPA), Bw. Emanuel Moirana anasema kipindi ambacho wanyamapori hususani tembo wanahamia kukidhi mahitaji yao husababisha uharibifu mkubwa katika vijiji wanavyopita.
Bw.Moirana anasema uharibifu huo ni pamoja na kuharibu Mazao, kuua mifugo na mara nyingine kuleta madhara kwa binadamu na hata kifo.
Anasema uharibifu ambao hufanywa na wanyamapori ni kuvamia mashamba katika maeneo wanayopita na maeneo yaliyokandokando ya hifadhi pamoja na kuvamia mifugo katika malisho na hata katika maboma.
Uharibifu mwingine ni wa miundombinu ya maji kama
mabomba,kujeruhi,kisababisha vifo kwa binadamu hasa jamii za wafugaji wanaojaribu kulinda mifugo yao ama wakulima ambao mara nyingi hushambuliwa wakiwa mashambani.
Anasema sababubu inayochangia migogoro baina ya wanyama pori na binadamu ni mapitio ya wanyama kuvamiwa na kukaliwa na binadamu pamoja na ongezeko la idadi ya watu katika maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyama na uhamaji wa kawaida wa wanyama hao.
Aidha anaeleza kuwa wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuwadhibiti wanyama hao ikiwa ni pamoja na kuweka uzio wa waya wa umeme,uzio wa miti mifano ya Michongoma,kuchimba mitaro kuzunguka eneo husika pamoja na kutumia pilipili.Anasema njia nyingine ambayo wanatumia kuwadhibiti wanyama hao ni kufanya doria za kufukuza wanyama hao na kuwasumbua ambapo askari hufanya doria mara kwa mara aidha kwa miguu au kwa gari kuzungukia eneo lililo na wanyama na kuwafukuza kwa kuwatishia kwa risasi za moto na risasi baridi.
Aidha anasema ili kuweza kudhibiti wanyama hao serikali za vijiji zinapaswa kuwa na mpango bora wa matumizi ya Ardhi na kuutekeleza.Anasema mpango huo uainishe maeneo maalumu kwa ajili ya makazi ya raia,maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo,maeneo ya Kilimo pamoja na maeneo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi maliasili
“Utekelezaji wa mpango huu utasaidia kuepusha migogoro inayotokana na migogoro kati ya wanyama na binadamu”anasema Bw.Moirana.
Bw. Moirana anasema pamoja na jitihada mbalimbali walizonazo za kudhibiti wanyamapori wasivamie katika mkazi ya watu,wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo bajeti kuwa finyu ikilinhanishwa na shughuli za kupambana na wanyama hao waharibifu.
Chanzo;
Flora Temba,Majira (Julai,2011)
Thursday, July 7, 2011
UJASIRIAMALI NA NAMNA YA KUTENGENEZA MITANDAO
Ujasiriamali ndio neno jipya. Kila mtu anaongelea habari za ujasiriamali. Pengine hii inatokana na wengi wetu kutambua kwamba nyakati zimebadilika na ujasiriamali ndio njia iliyo sahihi zaidi kama mtu anatamani mafanikio ya kweli maishani.Vijana ndio chachu zaidi ya ujasiriamali au naweza kusema ndio wanategemewa zaidi kuendeleza ujasiriamali hususani katika ulimwengu wa leo wa sayansi na tekinolojia.
Pamoja na nia nzuri walizonazo vijana, pengine ukiwemo wewe unayesoma makala hii, kipo kizingiti ambacho ni lazima watu wajifunze mbinu mpya za kukivuka. Kizingiti hicho ni aina ya elimu itolewayo mashuleni. Kwa bahati mbaya elimu zitolewazo mashuleni bado hazijawekwa katika msingi unaomuwezesha kijana kujiajiri au kwa maneno mengine kuwa mjasiriamali pindi amalizapo masomo yake.
Bado tupo katika ule mfumo wa kikoloni. Ukimaliza shule unachotakiwa ni kuanza kutafuta kazi. Zunguka jijini Dar-es-salaam kwa mfano, utakutana na vijana wengi wasomi waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini wakiwa wamebeba vyeti vyao kwenye vijifuko vya plastiki wakizurura kusaka ajira. Hakuna anayefiria kujiajiri kwa kutumia elimu aliyoipata chuoni. Kwanini? Ndivyo ilivyo. Elimu aliyopewa haikumuandaa.Utakutana na engineer wa umeme ambaye hajawahi kubadilisha hata balbu!(nimeongeza chumvi kidogo hapa lakini kuna ukweli ndani yake!) Amesomea nadharia zaidi ya vitendo. Utakutana na mwanafunzi mhitimu wa masomo ya kilimo na mazingira ambaye hajui shamba ni nini.Hilo ni kosa katika mfumo wetu wa elimu. Ni lazima serikali ichukue jukumu la makusudi kubadili mfumo huo.
Lakini wapo wengine wengi ambao wana nia ya kweli ya kuwa wajasiriamali. Wana nia ya kujiajiri. Leo tutaangalia jinsi gani mjasiriamali chipukizi aanzishe kampeni yake. Si ushasikia kwamba biashara siku hizi ni kujuana? Ujasiriamali pia. Ni muhimu sana kujua ni nani au ni wapi uende endapo mambo yatakwama. Siongelei wapi uende kutoa au kupokea rushwa.La. Nataka kuongelea kitu kinachoitwa na wenzetu wa magharibi “networking”.Kwetu sisi hiki ndicho tunachoita “mtandao”.Mitandao ya kijamii kama vile facebook,twitter,myspace nk ni sehemu nzuri ya kutengeneza network.Itumie vizuri.
Ni muhimu kutengeneza mtandao mzuri kama unataka kuwa mjasiriamali makini na hususani kama unataka kufanikiwa. Kumbuka kwamba hapa hatuongelei kubadilishana business cards peke yake bali kumjua mtu kwa nia njema ya kusaidiana.Kumbuka neno ni “kusaidiana” na sio wewe pekee kupokea msaada.Lazima pawe na nia njema ya kusaidiana.
Kabla sijaanza kuorodhesha mbinu mbalimbali za kutengeneza ‘mtandao’ wako, naomba nikwambie kwamba siri ya kwanza ya kuanza kuwa mjasiriamali ni maandalizi.Jiandae kwa mtaji,elimu(ya darasani na mtaani),mbinu za kibiashara nk. Pili hakikisha kwamba una mapenzi ya dhati na hicho unachotaka kufanya.Usiingie kwenye biashara au ujasiriamali kwa sababu tu umemuona fulani amefanya hivyo.Kuna umuhimu mkubwa wa kujitambua katika suala zima la ujasiriamali. Baada ya kusema hivyo,sasa tuingie kwenye maeneo ya kutengeneza mtandao wako kama mjasiriamali;
■ Washindani wako: Biashara ni ushindani lakini sio uadui.Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio ni vizuri sana ukawajua washindani wako wa kibiashara.Pata vipeperushi vyao,tembelea tovuti zao,wajue wateja wao na kwanini hao watu ni wateja wao.Kisha jitambulishe kwao.Najua hapa unasema;nijitambulishe?!! Ndio,jitambulishe.Kama nilivyosema ni washindani lakini sio maadui zako. Mshindani wako anaweza kukufaa pia.Anaweza kuzidiwa na kazi akakusukumia zingine.Jitambulishe,jenga uhusiano mzuri wa kibiashara.Isitoshe nyote mpo kwenye biashara moja,sekta moja.Ya kesho hamyajui.Kama kuna chama au ushirika wa watu waliomo kwenye eneo lako la ujasiriamali,jiunge.
■ Vyombo vya Habari: Siku hizi kuna aina nyingi zaidi za vyombo vya habari na mawasiliano. Kuna magazeti,televisheni,radio, blogs nk. Kama mjasiriamali,ni muhimu ukajuana na watu wanaoendesha au hata kumiliki vyombo hivi vya habari. Na zaidi angalia vile ambavyo vipo karibu zaidi na eneo lako la ujasiriamali.Ni rahisi zaidi kwa habari ya ujasiriamali wako kuandikwa gazetini,kuongelewa radioni,kuonekana kwenye televisheni nk kama watu wa vyombo vya habari wanajua unachofanya.Mara nyingi watu wengi wa habari wanapotaka kufanya utafiti wa jambo fulani huanza kwanza kwa kuangalia “sources” alizonazo. Kumbuka kwamba kuandikwa mara kwa mara juu ya kazi zako,ujasiriamali wako, husababisha watu kukukumbuka,kukuheshimu na hivyo kuwa rahisi kwao kufanya biashara na wewe.
■ Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO): Mjasiriamali makini ni yule ambaye anadhamiria kuisaidia jamii yake kwa njia moja au nyingine. Zipo faida mbalimbali za kibiashara kwa mjasiriamali ambaye hurudi nyuma na kusaidia jamii yake.Kuna faida za mapunguzo au unafuu fulani wa kodi(waulize TRA watakupa data zaidi).Isitoshe jamii iliyo bora,iwe kiafya,kielimu nk ni wateja wako wazuri wa siku za mbeleni.
Hivyo ni muhimu kujuana na watu mbalimbali wanaoendesha mashirika yasiyo ya kiserikali ama NGOs.Dhamini shughuli zao mbalimbali.Ukifanya hivyo(mara nyingi ni bei rahisi zaidi) unakuwa umesaidia jamii yako na pia umetangaza biashara yako.Lakini kuwa makini. Zipo NGO kibao siku hizi.Nyingine ni mitaji ya watu.Achana nazo.Tafuta zile ambazo ni halali na kazi wanayofanya inaonekana katika jamii.
■ Mwanasheria mmoja au wawili: Kama ilivyo katika maeneo mengine,msaada wa kisheria unaweza ukahitajika wakati wowote katika ujasiriamali.Unaweza kutaka ushauri,unaweza kushitakiwa nk. Ni vizuri kama ukawa unajuana na watu mbalimbali waliopo kwenye uwanja wa wanasheria. Mara nyingi watu tunaelewa mambo vizuri tunapokuwa tunaongea na watu ambao tunafahamiana nao kwa njia moja au nyingine.Wazungu wanasema unakuwa “more comfortable”. Sasa kwa sababu huwezi jua ni lini utahitaji msaada wa kisheria, ni vizuri ukajuana na mwanasheria mmoja au wawili kwa minajili ya kukusaidia endapo utaalamu wao utahitajika.
Kumbuka tu kwamba hapa siongelei msaada wa bure bali malipo fulani ingawa kutokana na kujuana huko,ni rahisi kupata punguzo la bei na pia ile faraja ya kuongea na mtu unayejuana naye.Wakati mwingine unaweza kumuuliza tu “rafiki mwanasheria” kuhusu hoja fulani ya kisheria wakati wa chakula cha mchana(lunch) na ukawa umepata jibu.
■ Mwakilishi wako wa kisiasa: Bahati mbaya au nzuri ni kwamba hakuna biashara au ujasiriamali ambao unaweza kujitenga moja kwa moja na siasa za nchi au eneo fulani. Kuanzia kwenye ugawaji wa maeneo ya biashara, utolewaji wa leseni za biashara,sera mbalimbali za biashara nk lazima kuna ’siasa’ fulani. Sasa kwa sababu sera hizo huwa zina mkono wa siasa,ni muhimu sana kujuana na wahusika au watungaji wa sera hizo ambao mara nyingi ni wanasiasa.Ukiwajua au kujuana na wanasiasa wa eneo lako,ni rahisi kwako wewe kufikisha ujumbe,malalamiko yako na pia hisia zako katika mambo mbalimbali.Kumbuka kwamba biashara au ujasiriamali wako ni sehemu ya jamii.Ni muhimu ukamjua Balozi,Mjumbe,Mbunge,Waziri nk kutoka katika jumuiya yako au mahali ilipo biashara yako.Usije kujidanganya kwa kusema ‘ah mimi sitaki kabisa kujuana na wanasiasa”.Utakuwa unakosea na utakuwa sio mjasiriamali makini.
Kwa ufupi hayo ni maeneo ambayo ni muhimu kuyazingatia endapo “ujasiriamali” ni kitu ambacho unakitamani au tayari unakifanya. Lakini kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza katika makala zangu; fanya kazi kwa bidii na maarifa. Hiyo ndio siri ya msingi ya mafanikio katika maisha. Kujuana na watu mbalimbali muhimu peke yake haitoshi. Kazi mbele. Tukutane wiki ijayo.
Chanzo: www.bongocelebrity.com.
KILIMO NA MAENDELEO YA TANZANIA
Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Kilimo kinachukua takribani nusu ya pato zima la taifa na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nchi za nje. Pamoja na kutoa chakula, kilimo vile vile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania. Sehemu kubwa ya kilimo Tanzania ni cha wakulima wadogo-wadogo (small-holder farmers, au peasants) ambao mashamba yao yana ukubwa wa kati ya hekta 0.9 na hekta 3.0 kila moja. Karibu asilimia 70 ya ardhi ya ukulima wa mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 kwa kutumia maksai na asilimia 10 kwa kutumia trekta. Kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua. Uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaoongoza katika uchumi wa Kilimo. Hekta milioni 5.1 zinalimwa nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula tu. Wanawake ndiyo wafanyakazi wakubwa mashambani. Matatizo makubwa yanayokabili Kilimo nchini Tanzania ni upungufu wa nguvu kazi na uzalishaji kutokana na uhaba wa nyenzo za kisasa za ukulima pamoja na kutegemea sana hali ya hewa ambayo haiaminiki. Mazao na wanyama huathirika vibaya sana nyakati za ukame. Kilimo cha umwagiliaji maji ndicho ambacho kinaweza kuinusuru Tanzania katika kuhakikisha uzalishaji usioterereka ili kujenga akiba nzuri ya chakula, pamoja na kuongeza kipato na kuboresha uzalishaji wa mazao kwa mkulima.
Uzalishaji Katika Kilimo
Pato la ndani ya nchi la Kilimo limekuwa kwa kiwango cha asilimia 3.3 kwa mwaka kuanzia mwaka 1985. Mazao ya chakula yaliongezeka kwa asilimia 3.5, na mazao ya biashara kwa asilimia 5.4 kwa mwaka. Serikali ya tanzania inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Vilevile inatilia maanani vichocheo vyote vinavyotoa msukumo wa uzalishaji katika kilimo kama vile miundombinu, huduma za fedha vijijini, umilikaji ardhi na utawala bora. Ili kufanikisha azma hiyo, hatua mbalimbali sasa hivi zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika kilimo kwa wakulima wadogowadogo na wale wakubwa wa kibiashara. Serikali vilevile inajitahidi kuongeza mgao wake wa bajeti kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya kilimo kwa ujumla.
Mazao ya Chakula
Tanzania imejaliwa kuwa na aina nyingi za kilimo kutegemeana na hali ya hewa na mazingira ya nchi. Mazao makubwa ya chakula ni: mahindi, mtama, mpunga, ngano, maharage, muhogo, viazi na ndizi.
Mazao ya Biashara
Kahawa, pamba, korosho, tumbaku, katani, alizeti, majani ya chai, karafuu, mazao ya bustani, ufuta, viungo vya chakula na maua.
Maeneo ya Kilimo
Nyanda za pwani, mabonde na safu za milima ya mashariki, nyanda za juu za kusini, Bonde la ufa la Kaskazini, milima ya volkeno, Bonde la Kati, Rukwa – Bonde la Mto Ruaha, sehemu za matope za bara, ufipa na Nyanda za Juu za Magharibi.
Kilimo cha Kumwagilia Maji
Tanzania inao uwezo wa kuendeleza kilimo cha kumwagilia ili kuwa na uhakika wa akiba ya chakula ya kudumu pamoja na kuboresha viwango vya maisha ya watu wake. Maji yanapatikana kwa wingi katika mito mikubwa na midogo pamoja na maziwa na mabwawa. Eneo ambalo linaweza kuwekwa chini ya kilimo cha kumwagilia maji ni hekta milioni 1.0, lakini mpaka hivi sasa ni hekta 150,000 tu zinazolimwa kwa kumwagilia maji.
Uwekezaji katika Kilimo
Mashirika yafuatayo, ambayo yako chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula, ni vitega uchumi vizuri vya uwekezaji kwa wale wanaotaka kuyanunua, au kuingia ubia na Serikali.
• Shamba la Kahawa la Mbozi lenye eneo la hekta 409.32. Mashamba haya yako Ishera, Ndungu, Tukumbi, Ng’amba, Ihanda na Hauseketwe.
• Kampuni ya Korosho na viwanda vyake vilivyoko Mtwara, Kibaha, Likombe, Masasi, Newala, Tanita dar es Salaam, Lindi, Nachingwea na Tunduru.
• Kampuni ya Usagishaji ya Taifa na vinu vyake vilivyoko Isaka, Tabora, Shinyanga, Mtwara na Iringa (vyote vya mpunga); na vinu vingine vya mahindi na mtama vikiwa Mwanza, Mtwara na Arusha. Mali za kampuni ni pamoja na majengo ya kuishi.
• Kampuni ya Mashamba Bagamoyo (Bagamoyo Farms Ltd.).
• Kampuni ya Mbegu ya taifa (Shamba la Kwamtili).
• Mashamba ya Mpunga ya Dakawa na Mbarali, mashamba ya mahindi ya Ruvu na miradi ya Kapunga, Madibira, Mbozi na Namtumbo.
• Mashamba ya Ngano na Karakana Basutu, Gawal, Gidagamwd, Mulbadaw, Murandja, Kampuni ya Ngano ya Seteet, Warret na Kituo cha kati cha matengenezo ya Ufundi (CMSC).
• Mashamba ya sukari yanayomilikiwa na Chuo cha Sukari cha Taifa na Kampuni ya Sukari ya Kagera.
• Viwanda vya mazao ya Kilimo.
Chanzo: www.tanzania.go.tz/kilimo.html