Pages

Friday, April 1, 2011

UMAKINI KATIKA KUFANYA MAAMUZI

Kufanya maamuzi ni kuchagua jambo gani muhimu ulifanye katika muda huo huku ukiacha kufanya mambo mengine kwa wakati huo huo.Kila binadamu kwa wakati mmoja au mwingine hukumbwa na tatizo la kutoa maamuzi sahihi katika kila dakika na saa anayoishi.Hatima ya kila mwanadamu hutegemea sana maamuzi anayofanya.Hivyo inahitaji umakini na utulivu wa hali ya juu unapofanya maamuzi. Maamuzi unayofanya kwa sekunde moja bila kujali kitu chochote yanaweza kubadili maisha yako yote kwa wakati huo au kwa wakati ujao.

Ugumu wa kufanya maamuzi unaonekana zaidi katika maswala ya maendeleo.Binadamu katika maendeleo ni lazima afanye maamuzi,maamuzi hayo anaweza kuyafanya mwenyewe au kwa kuwashirikisha watu wengine.Wakati mwingine inakuhitaji ufanye maamuzi wewe kama wewe na wakati mwingine inakubidi uwashirikishe watu wengine.Katika mambo ya maendeleo inashauriwa baada ya kutafakari mwenyewe ni maamuzi gani uyafanye, kabla ya kufanya maamuzi hayo ni vyema ukawashirikisha na watu wengine ili ufanye uamuzi wa busara na yenye mafanikio kwako na kwa watu wanaokuzunguka(jamii kwa ujumla).

Maswali yafuatayo yanaweza kupelekea maamuzi makubwa ya maendeleo katika maisha..mfano shule au chuo gani nisome?,nisome nini?,nifanye biashara gani?,nifanye kazi ipi,niishi wapi?,nimchague kiongozi gani? nk..Wakati mwingine muda unaweza ukaathili maamuzi unayofanya kwa kuchelewa kufanya maamuzi au kuwahi. Ipo mifano mingi ya watu mbalimbali (ikiwemo mimi) waliopata matokeo mazuri au mabaya baada ya kuwahi au kuchelewa kufanya maamuzi. Ila swala la muhimu ni umakini gani unatumika katika kufanya maamuzi.

Zifuatazo ni njia tano(5) muhimu unazoweza kutumia katika kufanya maamuzi:-
• Kwanza,kutambua jambo lipi unataka kulifanyia maamuzi
• Jambo hilo lina umuhimu kiasi gani na matokeo yake ni yapi katika maisha yako na ya jamii.
• Maamuzi hayo yanauharaka kiasi gani (muda wa kutoa maamuzi)
• Ni muhimu kufanya maamuzi peke yako au uwashirikishe watu wengine
• Ni akina nani uwashirikishe katika kufanya maamuzi (mf wafanyakazi wenzako,wanafunzi wenzako,wazazi/walezi, au wataalamu waliobobea katika mambo ya ushauri)
Maendeleo ni mchakato unaoshirikisha uwezo wa mtu binafsi akishirikiana na watu wengine katika kufanya maamuzi yenye tija katika maisha. Ni vyema kutafakari kabla ya kufanya maamuzi yenye matokeo makubwa katika maisha yetu na maisha ya watu wengine wanaotuzunguka. Fumbuka fanya maamuzi ya busara.

Na.
Mbele,Innocent John

No comments:

Post a Comment